Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wameendesha mafunzo maalum kwa watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita, kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kugawa majiko ya gesi yenye mitungi ya kilo 6.
Waliofaidika na mpango huu ni jumla ya watu 64 wenye mahitaji maalum, wakiwemo wasioona, wenye ualbino, na wenye usikivu hafifu. Mafunzo haya yamefanyika sambamba na kampeni ya serikali ya kuhakikisha makundi yote katika jamii yanapata fursa ya kutumia nishati safi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Ally Mketo, ameishukuru REA kwa kuendesha mafunzo hayo na kusisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya nishati safi ili kuboresha maisha na afya ya walengwa.
Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka REA, Mhandisi Kelvin Tarimo, amesema lengo la serikali ni kuhakikisha nishati safi ya kupikia inawafikia makundi yote, ikiwemo watu wenye ulemavu. Ameongeza kuwa mpango huu ni sehemu ya jitihada za kupunguza matumizi ya nishati mbadala zisizo salama na zinazochangia uharibifu wa mazingira.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA), Kelvin Nyema, pamoja na Mwenyekiti wa Wasioona Wilaya ya Bukombe, Rosemary Nuhu, wameelezea manufaa waliyopata kutokana na mafunzo hayo. Wamepongeza juhudi za REA katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanajengewa uwezo wa kutumia nishati salama na rafiki wa mazingira.
Mpango huu wa REA ni sehemu ya dhamira ya serikali ya kuhakikisha wananchi wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum, wanapata nishati salama na endelevu.