Home Kitaifa TBS YATOA WITO KWA WAZALISHAJI WA BIDHAA KUHAKIKISHA WANAWEKA TAARIFA SAHIHI KATIKA...

TBS YATOA WITO KWA WAZALISHAJI WA BIDHAA KUHAKIKISHA WANAWEKA TAARIFA SAHIHI KATIKA VIFUNGASHIO KUMLINDA MTUMIAJI

Na Mwandishi Wetu.

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wazalishaji wa bidhaa nchini kuhakikisha wanaweka taarifa kwenye vifungashio vya bidhaa husika ili kumuwezesha mlaji kutambua bidhaa husika ni bora au si bora kwa matumizi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 26, 2024 Jijini Dar es Salaam, Afisa Udhibiti Ubora, Moses Mbambe amesema ni muhimu wazalishaji kuweka taarifa kwenye bidhaa zao kwani taarifa hizo ni mawasiliano baina ya mzalishaji wa bidhaa pamoja na watumiaji wa bidhaa.

Amesema watumiaji wa bidhaa husika wanatakiwa kuzisoma taarifa hizo zilizopo kwenye vifungashio vya bidhaa husika kabla ya kununua na kwenda kuzitumia ili kumuwezesha kutambua ubora wa bidhaa hiyo na kutambua kama itamfaa kwa matumizi.

“Udhibiti ubora na usalama wa bidhaa ni jukumu shirikishi ambalo linaanzia kwa wazalishaji mpaka kwa walaji. Na suala la uwekaji wa taarifa kwenye bidhaa lipo kwa mujibu wa sheria na linaongozwa na viwango vya bidhaa husika”. Amesema Mbambe.

Aidha amesema taarifa muhimu ambazo zinatakiwa kuwepo kwenye bidhaa mbalimbali ni pamoja na muda wa kuisha kwa matumizi na lini bidhaa hiyo imetengenezwa kwani itasaidia kuepuka kununua bidhaa ambazo hazina ubora na kujiepusha na athari ambazo zinaweza kujitokeza kwa kutumia bidhaa ambazo zimekwisha muda wa matumizi.

Amesema taarifa zingine ambazo zinatakiwa kuwekwa kwenye vifungashio vya bidhaa husika ni pamoja na vitu ambavyo vimechanganywa wakati wa utengenezaji wa bidhaa husika ili kumsaidia mlaji au mtumiaji kuepuka kula au kutumia vitu ambavyo huwa hatumii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!