Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya juhudi mbali mbali za kupambana na tatizo la ajira nchini hasa kwa vijana
Ameyasema hayo Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe Mudrik Ramadhan Soraga wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki Mhe. Suleiman Haroub Suleiman kuhusu mikakati ya Serikali ya kuwasaidia wananchi kunufaika na fursa mbali mbali ikiwemo ajira, katika kikao cha kwanza cha Baraza la kumi la Wawakilishi huko Chukwani Mkoa wa Mjini Magharib Unguja
Amesema Serikali inatambua uwepo wa changamoto hiyo hasa kwa vijana hivyo inaendelea kuchukua hatua mbali mbli ya kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kuanzisha Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa lengo la kuimarisha sekta ya ujasiriamali ikiwemo mafunzo, miundombinu ya uwezeshaji, mitaji kwa njia ya mikopo pamoja na kuwatafutia masoko ya kuuzia bidhaa zao ndani na nje ya nchi
Aidha Waziri Soraga amesema Wizara yake kwa kushirikiana na taasisi mbali mbali za Umma, Binafsi na Washirika wa Maendeleo ikiwemo Shirika la Kazi Duniani (I.L.O) iendelea kutekeleza programu za kukuza ujuzi kwa vijana ili waweze kujiajiri na kuajirika
“Serikali imeandaa programu mbali mbali ikiwemo mafunzo kazi (Apprenticeship), na mafunzo ya muda mfupi ya kukuza ujuzi (NEET – Not in Employment, Education of Training) yenye lengo la kuwaongezea ujuzi vijana katika kujikita na fani mbali mbali za ajira ili bidhaa zao ziwe na ubora na zitambulike ndani na nje ya nchi.” Alisema Soraga
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kujenga vyuo vya amali ili kuwajengea ujuzi vijana na changamoto iliyopo ya vijana wengi kukosa ujuzi unaohitajika katika soko la ajira hivyo vyuo hivyo vitahakikisha vinatoa elimu sahihi itakayowasaidia wananchi wote wakiwemo wa Jimbo la Kiembesamaki kunufaika na fursa za uwekezaji zilizopo nchini.
Vikao vya Baraza la wawakili vinatarajiwa kuendelea tena hapo kesho Septemba 8 2022.