Home Kitaifa ZAIDI YA WATU MIL 1.2 WANATARAJIA KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA...

ZAIDI YA WATU MIL 1.2 WANATARAJIA KUJIANDIKISHA KWENYE DAFTARI LA WAPIGA KURA MKOANI PWANI -RC KUNENGE

Mkoa wa Pwani unatarajia kuandikisha zaidi ya watu milioni 1.2 kwenye daftari la wapiga kura, zoezi ambalo limeanza rasmi Oktoba 11 na linatarajiwa kukamilika Oktoba 20 mwaka huu.

Kwa mujibu wa mkoa huo ,zoezi hilo litafanyika katika vituo vya uandikishaji 2,374 vilivyopo kwenye Vitongoji 2,028, Vijiji 417, na Mitaa 73.

Akiongoza wananchi katika zoezi hilo la uandikishaji kwenye Daftari la Wapiga Kura, lililofanyika Mtaa wa Mkoani A, Kata ya Tumbi, Wilaya ya Kibaha, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, alieleza mwamko ni mkubwa na amewapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi.


"Ngazi ya mkoa tumezindua zoezi hili nikiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta, na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Simon, Nashukuru kuona idadi kubwa ya wananchi kwani ni saa 2 asubuhi naamini baadaye mwamko watu watakuwa wengi zaidi," alieleza Kunenge.

Kunenge alifafanua kuwa kujiandikisha ni haki ya msingi, na hatua hiyo itawawezesha wananchi kupiga kura kuchagua viongozi wanaowafaa ifikapo Novemba 27 mwaka huu.

“Maendeleo yanaanzia kwenye jamii tunayoishi, Msingi bora wa maendeleo huanzia ngazi za mwanzo, na viongozi wa mwanzo ni wale tuliowachagua kwenye maeneo yetu,” alisisitiza Kunenge.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Tumbi, Msemakweli Kalia, alisema kuwa hamasa ni kubwa, ikionyesha namna wananchi wanavyotambua haki zao hata katika masuala ya kitaifa.

Alieleza kuwa kata hiyo ina wakazi wapatao 15,641, na wanatarajia kuandikisha takriban wakazi 8,000.

“Naomba kuwaelimisha wananchi wajue kwamba zoezi hili ni la kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura, na si kwa ajili ya kuchukua vitambulisho,”. Ni zoezi la haraka, halichukui muda mwingi” alieleza Msemakweli.

Baadhi ya wakazi waliojitokeza kujiandikisha katika Mtaa wa Mkoani A, Emmanuel Masela na Saumu Almas, walisema walifika kwenye kituo kabla ya saa 2 asubuhi na wanashukuru kuungana na kiongozi wa mkoa katika zoezi hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!