Na Magrethy Katengu– Dar es salaam
Wanawake Nchini hususan Vijana wa kike ( Wasichana) wametakiwa kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za Uongozi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba mwaka huu na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani ili kuwa Sehemu ya kufanya maamuzi katika masuala mbalimbali ya Jamii na Taifa.
Wito huo umetolewa leo Oktoba 10,2024 Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Watoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mathias Haule katika Kampeni ya kuhamasisha Watoto wa Kike kushika hatamu za Uongozi iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Plan kwa lengo la kuwajengea Uwezo.
“Tunahamasisha wazazi wenye watoto kuwahimiza vijana wao wa kike kushiriki kuwania nafasi katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu kwani nao wana maono makubwa na wapate uzoefu kutatua masuala yanayoihusu jamii”amesema Haule
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika hilo la Plan Jane Sembuche amesema Watoto zaidi ya 40 wamefanyakazi kama Viongozi katika Taasisi na Balozi mbalimbali na wamengewa uwezo wa kutosha na hivyo wanaamini wengi wao watatimiza ndoto za kuwa Viongozi huku akisema jitihada za kumsaidia Mtoto wa kike zimekuwa na mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali.
“Siku yetu ya leo ambayo tunaiita Girls takeover au wasichana kushika hatamu ni kampeni ambayo Plan International Tanzania ikiwemo na Nchi mbalimbali Duniani ambapo Plan ina ofisi hua tunafanya kila mwaka tunasherehekea siku ya watoto wa kike duniani ambayo hufanyika Oktoba 11 ” amesema.
Aidha amesema kuwa wasichana wanaweza kuwa viongozi wazuri katika jamii,kitu cha msingi ni kuweka juhudi , malengo na kujiamini yeye kama msichana anaweza kufikia malengo yake na anaweza kua kiongozi katika jamii na kuleta mabadiliko yanayotakiwa.
Akizungumzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba mwaka huu Mkurugenzi huyo Mkazi wa Plan International Tanzania amesema kuwa pamoja na shirika hilo kutekeleza Kampeni ya Girls takeover lakini pia lina kampeni nyingine ya “Sikia Sauti zetu ” ili kuwezesha sauti za wasichana sehemu mbalimbali wanahamasika kuzungumza nakuleta changamoto zao sehemu husika zipatiwe ufumbuzi
Nao baadhi ya Wasichana kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es salaam walioshiriki katika Kampeni hiyo pamoja na Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari kutoka Mkoa wa Katavi wamesema wamejifunza mambo mengi katika Kampeni ikiwa ni pamoja na kutumia muda vizuri huku wakitoa wito kwa Wasichana wanatamani kuwa Viongozi kuongeza bidii na kutokata tamaa.
Naye mwanaharakatu wa elimu kwa mabinti Moureen Mkambala ametoa wito kwa jamii kutoa nafasi kwa mwanamke nao wanajua kuongoza na kuleta mabadiliko makubwa kwenye jamii.
Naye Mkurugenzi wa hospitali CCBRT Muuguzi Careen Gilbert amesema yeye amekuwa akikutana na wanawale ambao wanaugua fistula waliokata tamaa na ametumia muda wake kuwatia moyo kwamba ugonjwa unatibika wasijifungie majumbani kwani wao nao wanategemewa.
Kampeni hiyo ni sehemu ya kuelekea Maadhimisho ya Mtoto wa Kike Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba 11.