Home Kitaifa ZOEZI LA SENSA YA WANYAMAPORI LAZINDULIWA RASMI LEO MKOANI MOROGORO

ZOEZI LA SENSA YA WANYAMAPORI LAZINDULIWA RASMI LEO MKOANI MOROGORO

Na Happiness Shayo-Morogoro

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana amezindua rasmi zoezi la Sensa ya Wanyamapori lengo ikiwa ni kuhesabu Wanyamapori nchi nzima kwa uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori, misitu ma kuendeleza utalii.

Uzinduzi huo utakaogharimu takribani shilingi milioni 560 katika mfumo wa Ikolojia ya Nyerere – Selous – Mikumi yenye kilomita za mraba 104,143 umefanyika katika eneo la Matambwe kwenye Hifadhi ya Taifa ya Nyerere leo Oktoba 5,2024 Mkoani Morogoro.

“Zoezi hili linathibitisha jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori na misitu nchini na kuendeleza utalii” Mhe. Chana amesema.

Amesema Sensa hiyo katika ikolojia ya Nyerere – Selous- Mikumi ni sensa ya 17 tangu kuanza kuhesabu Wanyamapori katika eneo hilo na litafanyika kuanzia tarehe 5 Oktoba 2024 hadi Novemba 14, 2024.

Akizungumzia mchango wa sekta hiyo kwa Taifa, Mhe. Chana amesema kupitia uhifadhi Sekta ya Maliasili na Utalii inachangia asilimia 21% ya pato la Taifa, asilimia 25% ya fedha za kigeni, kuzalisha ajira takribani milioni 1.6 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Amefafanua kuwa Sensa hiyo itahusisha maeneo ya hifadhi za Taifa za Nyerere, Mikumi, Mapori ya Akiba, Selous, Lukwika-Lumesule, Liparamba na Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za Chingolie, Iluma , JUKUMU, Kisungule, Kimbanda, Mbaran’gandu, NALIKA-Tunduru, Ngarambe-Tapika, Liwale na Maeneo ya wazi yanayozunguka mfumo wa Ikolojia hiyo.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Dkt. Eblate Mjingo amesema sensa ya wanyamapori huonyesha viashiria ambavyo ni changamoto kwa wanyamapori na huisaidia Serikali kutenga rasilimali kwa ufanisi kukabiliana na ujangili, kuendeleza na kukuza utalii pamoja na kupunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori.

Zoezi hilo linafanyika kwa ushirikiano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zikiwemo TANAPA na TAWA chini ya uratibu wa TAWIRI.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!