Na Shomari Binda-Musoma
MKUU wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amewataka washiriki wa shindano la Miss Kanda ya Ziwa kuwa mabolozi wa utalii wa ndani.
Kauli hiyo imetolewa kwa niaba yake leo agosti 18,2024 ukumbi wa Le Grand Beach na mkuu wa Wilaya ya Rorya Juma Chikoka baada ya kumaliza ziara ya siku 4 kutembelea vivutio vya mkoa wa Mara.
Amesema mkoa wa Mara na Kanda ya Ziwa zipo fursa nyingi za utalii ambazo watanzania pia wanapaswa kuzitembelea.
Mwakilishi huyo wa mkuu wa mkoa amesema asilimia 75 ya Hifadhi ya Serengeti ipo mkoa wa Mara hivyo wananchi wa mkoa wa Mara na kanda ya ziwa wanapaswa kuhamasishwa kufanya utalii wa ndani.
Amesema licha ya utalii wa hifadhini mkoa wa Mara na kanda ya ziwa upo utalii wa madini na ziwa victoria ambao unapaswa kutangazwa.
“Mkuu wa mkoa anawapongeza sana kwa kutembelea fursa zilizopo mkoa wa Mara na sasa mkawe mabalozi wazuri kwa kuwa mmejionea wenyewe.
” Bado watanzania wanatakiwa kuhamasishwa kufanya utalii wa ndani na nyie mkawe mabalozi na mkafanye vizuri kwenye mashindano yenu na baadae Miss Tanzania”,amesema.
Meneja wa Le Grand Hotel ambao ni moja ya washiriki wa mashindano ya Miss Lake Zone amewataka washiriki hao kuwa mfano mzuri kwa jamii.
Amesema urembo ni taaluma na washiriki watumie fani ya urembo kujitangaza na kuutangaza utalii.
Kwa upande wao washiriki hao wamesema wataenda kuwa mabalozi wazuri katika kutangaza utalii wa ndani.