Na Mariam Muhando _Dar es salaam.
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Ilala imeridhishwa na Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ya Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam inayopelekea kutatua changamoto zinazo wakabili Wananchi Jijini humo.
Tamko hilo limekuja mara baada ya Kamati hio kufanya Ziara ya ukaguzi wa Miradi ya maendeleo leo tarehe 15 Agosti 2024 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho chini ya Usimamizi wa Rais Dr Samia Suluhu Hassani.
Miradi iliyotembelewa na Kamati hiyo ni pamoja na Mradi wa Ujenzi wa ghorofa sita, wenye thamani ya shilingi Bilioni 30, ujenzi wa Barabara ya Bima – kimanga kiwango cha lami yenye urefu wa mita 400 wenye thamani ya milioni 593 ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mitaro na kuweka taa za kisasa, Ujenzi wa vyumba vya madarasa 20 na matundu ya vyoo 45 katika shule ya Sekondari Bonyokwa wenye thamani ya milioni 539.
Akizungumza na Wandishi wa Habari Katika Ziara hio Mwenyekiti wa CCM Ilala Said Side ameiagiza Halmshauri ya jiji la DSM kuhakikisha wanawachagua Wakandarasi wazawa wenye uwezo na uzoefu ,ili waweze kukamilisha Miradi kwa ubora na wakati, ili wananchi waweze kufurahia huduma.
“Hii inaonyesha ni jinsi gani Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM inavyotekelezwa kwa kasi hivyo niwaombe kukamilisha miradi ambayo bado inasuasua hasa barabara ya Bima -Kimanga kwani barabara hii ni muhimu kwa wakazi wa Tabata kwa usafirishaji,” Said Side amesema “
Wakati huo huo ametoa Wito kwa maeneo ya wazi yanayomilikiwa na Halmshauri waendelee kukaribisha Wawekezaji wawekeze ili kuongeza , ajira na mapato ya Nchi na Halmshauri kwa ujumla.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amesema watahakikisha Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam inaendelea kuwa kinara katika ukusanyaji wa Mapato kwa kushirikiana na Wawekezaji kwenye kuwekeza katika maeneo yaliopo Jijini humo.
“Viongozi tuna deni kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu fedha zote zilishatolewa, Hivyo ni matumaini yake kuona Miradi yote katika sekta za Elimu, Afya, na Barabara inakamilika kwa wakati,” amesema Mpogolo.
Mpogolo amewaasa Wasimamizi wa Miradi kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili kukamilisha miradi kwa manufaa ya wananchi wa Ilala na maeneo ya jirani.