Na Monica sibanda-Dodoma
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema kuwa moja ya madhara ya Kilimo cha bhangi na mirungi ni kuondoa uoto wa asili.
Hayo yamebainishwa na Afisa Elimu kutoka DCEA, Said Madadi wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya Kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
“Tupo kwenye maaonesho ya kitaifa Nanenane lengo ni utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusiana na madhara ya matumizi ya dawa za kulevya pamoja na wakulima kuacha kujihusisha na Kilimo cha bhangi na mirungi.
“Kwasababu miongoni mwa madhara makubwa yanayopatikana kwa kulima bhangi na mirungi ni kusababisha kuondoa uoto wa asili, kwani inapolimwa bhangi au mirungi ile miti au mazao mengine hayalimwi maeneo hayo. Maana yake wanafanya kama mazao mbadala ya chakula kwahiyo kuna hatari ya njaa baadae,” amesema na kuongeza:
“Kwahiyo tunawashauri na kuwaelekeza waone athari ya kulima na kujihusisha na biashara hizo. Kwamfano maeneo ambayo wanalima bhangi hakuna hii miti mikubwa ambayo inatumika kama sehemu ya utunzaji wa Mazingira. Na wanapolima maeneo hayo wanakata miti mikubwa, na sehemu kubwa wanazolima ni sehemu za milimani ambapo kufikika ni vigumu lakini ni sehemu ambapo uoto wa asili unatakiwa uwepo kwaajili ya kulinda Mazingira, kwahiyo tunawashauri watu kuliangalia hilo,”.
Hata hivyo, amebainisha athari kubwa ya matumizi ya mirungi ni kusababisha saratani, lakini pamoja na upungufu wa nguvu za kiume.
“Bangi inasababisha matatizo ya afya ya akili, vichaa na ndo maana mtaani mtu akiona anaokota makopo wanasema zile ni bhangi kwani katika moja ya dawa za kulevya ambazo zina kemikali nyingi kuliko dawa yoyote ina kemikali zaidi ya 400,” amesema.
Naye Mfamasia Mwandamizi kutoka DCEA, Upendo Chenya amesema moja ya jukumu walilonalo ni kunguza madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kupunguza uhitaji wa hizo dawa.
“Katika kupunguza madhara tunatoa tiba kwa watumiaji au waraghibu ambapo kwa kushirikiana na Wizara ya afya serikali imekuwa ikiboresha huduma za tiba katika vituo vya afya ambapo katika kila kituo cha afya au Hospital kuna kitengo cha afya ya akili. Na sasa kuna vituo zaidi ya 16 nchini na vimeweza kusajili zaidi ya watu 17,000 na watu wanapata Huduma hiyo ambayo inawasaidia…pia kuna huduma za kisaikolojia ili kuweza kumsaidia mgonjwa ambapo Huduma inatolewa bure,” amesema.
Mwishooo