Na Ritha Jacob – Mzawa Online DSM
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya CRDB Bank Foundation, Tullyesther Mwambapa, amepongeza jeshi la kusambaza tabasamu pamoja na washiriki wote wanaoendelea kuunga mkono CRDB Marathon. Amesema kuwa wameweza kufanikisha kuvuka mipaka na kufikia nchi jirani kama Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, tofauti na miaka mitano iliyopita.
Mwambapa ameyazungumza hayo wakati wa uzinduzi wa jezi za jeshi la kusambaza burudani leo, 1 Agosti 2024. Alisema kuwa mashindano hayo yatafanyika katika Viwanja vya Farasi (Green Oysterbay) tarehe 18 Agosti 2024.
“Tangu tumeanzisha mbio hizi miaka mitano iliyopita, jeshi letu limeendelea kukua na mwaka huu lengo letu ni kusajili wanajeshi 8,000 kwa Tanzania, 1,000 Burundi, na 1,000 Congo. Nashukuru kwa mwitikio mkubwa wa kujisajili,” alisema Tullyesther Mwambapa.
Mbio hizo nchini Tanzania zitafanyika tarehe 18 Agosti 2024, Burundi tarehe 11 Agosti 2024, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo tarehe 4 Agosti 2024. Washindi kutoka nafasi ya kwanza hadi ya sita watapata zawadi. Pia, watoto kupitia programu ya Junior Jumbo watapata scholarship na zawadi nyingine kutoka Junior Jumbo.
Mwambapa amesema, “Naomba tuendelee kujiandikisha na pia tuwaandikishe familia zetu, hasa watoto kupitia programu ya Junior Jumbo. Watapata zawadi nyingi na itakuwa kama mtoko wa familia.“