TANZANIA imepata dola za Marekani Bilioni 2.32 kwa kuuza tani milioni 1.57 za mazao ya matunda na jamii ya kunde huko China, India, Marekani, Pakistan na Brazil.
Hayo yamesemwa leo (Alhamisi, Agosti Mosi, 2024) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizungumza na viongozi na wananchi mbalimbali waliohudhuria ufunguzi wa Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Sherehe za Nanenane ya Mwaka 2024 katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
“Kwa upande wa kilimo, hadi kufikia Juni, 2024 Serikali imewezesha upatikanaji wa masoko katika nchi za China, India, Marekani, Pakistan na Brazil ambapo tani milioni 1.574 za mazao ya matunda na jamii ya kunde zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 2.329 zimeuzwa katika nchi hizo,” amesema.
Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imeingia makubaliano ya kuuza tani milioni 1.25 za mahindi. “Kati ya hizo, tani 650,000 zitauzwa Zambia; tani 500,000 zitauzwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na tani 100,000 kwa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa.”
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imewezesha upatikanaji wa soko la vanilla, pilipili manga, karafuu, nanasi, kakao, viazi mviringo, tumbaku na ndizi katika nchi za China, Marekani, Pakistani, Afrika Kusini na India ambayo yanatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.
“Kwa upande wa wafugaji, hadi Aprili, 2024 jumla ya tani 13,745 za nyama zenye thamani ya dola za Marekani milioni 56 zimeuzwa katika nchi za Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Rwanda, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Vietnam. Pia vipande 1,542,916 vya ngozi vyenye thamani ya shilingi bilioni saba vimeuzwa katika nchi za Nigeria, Togo, Kenya, Ethiopia na Pakistan.”
Kwenye sekta ya uvuvi, Waziri Mkuu amesema hadi kufikia Aprili, 2024, tani 41,271 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 134,572, wenye thamani ya shilingi bilioni 515.78, waliuzwa katika nchi za Umoja wa Nchi za Ulaya, Canada, Marekani, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, China, Zambia, Uganda na Malawi.
Akielezea jitihada ambazo zimechukuliwa na Serikali kuendeleza sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, Waziri Mkuu amesema sambamba na utashi na maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kuongeza ajira kwa vijana na wanawake kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyobora.
“Kupitia programu hiyo, vijana 686 wanaendelea na kilimo biashara katika mashamba ya pamoja na tayari wameanza uzalishaji. Kwa upande wa mifugo, vijana 161 wanaendelea na programu ya unenepeshaji wa ng’ombe katika vitalu vya Ranchi za Taifa (NARCO). Sekta ya uvuvi nayo haikuachwa nyuma tayari vijana 200 wamehitimu mafunzo na vijana 300 wanaendelea na mafunzo ya ukuzaji wa viumbemaji.”