Na Shomari Binda- Musoma
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) mkoa wa Mara imetakiwa kuendelea kutoa elimu kwa wanafunzi juu ya madhara ya Rushwa.
Kauli hiyo imetolewa na kiongozi wa mbio za mwenge Godfrey Mnzava leo julai 30 alipokuwa akizindua klabu ya wapinga Rushwa kwenye shule ya sekondari Kamnyonge.
Amesema Rushwa ina madhara makubwa kwenye idara mbalimbali hivyo ni muhimu wanafunzi kupata elimu juu ya madhara yake.
Mnzava amesema TAKUKURU mkoa wa Mara inafanya kazi nzuri ya uanzishwaji wa klabu kwenye mashule na vyuo na kusisitiza mkazo kwenye suala la elimu.
Kiongozi huyo wa mbio za mwenge amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt.Samia Suluhu Hassan anatoa fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali hivyo wanafunzi wanapaswa kuwa na utambuzi juu ya madhara ya Rushwa.
” Niwapongeze sana TAKUKURU mkoa wa Mara kwa kazi nzuri kwenye uanzishwaji wa klabu za wapinga Rushwa mashuleni na kwenye vyuo ili vijana wajue madhara ya Rushwa.
” Hawa vijana wetu wakiwa na elimu juu ya madhara ya Rushwa watakuwa mfano mzuri kwenye mapambano haya na baadae kuwa na taifa lisiro na waomba na wapokea Rushwa”,amesema.
Afisa elimu kwa umma wa TAKUKURU mkoa wa Mara, Amos Ndege amesema kwa shule za msingi wameanzisha klabu 55,sekondari 19 na vyuo vyote 5 vilivyopo klabu zimeshaanzishwa.
Amesema elimu itaedelea kufikishwa kwenye klabu hizo zilizoanzishwa na kuendelea kuanzishwa nyingine.
Baadhi ya wanachama wa klabu ya wapinga Rushwa kwenye shule ya sekondari Kamnyonge wamesema wamekuwa wakipewa elimu na TAKUKURU ambapo kwa sasa wanao uelewa juu ya Rushwa.