Na Ritha Jacob – Katavi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka wazazi kuwaacha watoto wenye umri wa miaka 15-19 wasome badala ya kuzaa, kwani wengi wao wanapata watoto wakiwa bado hawajafikia muda sahihi.
Akizungumza na wananchi wa mkoa huo mara baada ya kutembelea na Kuona Maendeleo ya Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi ikiwa ni sehemu ya ziara yake julai 14, 2024 amesema Watoto wapewe nafasi wakue kabla ya kuzaa Watoto wenzao.
“Nilipokwenda kwenye wodi ya kina mama, hasa watoto ambao hawajatimia, nimekuta mmoja tu ndiye mpevu, lakini wengine wote ni wenye umri wa miaka 15-19. Naomba sana, wapeni nafasii watoto wakue kidogo, waacheni waende shule Wapeni nafasi watoto wakue kabla ya kuzaa watoto wenzao.” Amesema
Aidha, Rais Samia aliwapongeza mganga mkuu na timu ya madaktari na wahudumu kwa huduma nzuri kwa wananchi wa Katavi, na amewataka kuendelea kuzingatia viapo vyao vya kutoa huduma kwa uadilifu.
Aidha, Rais Samia amewataka wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote ili kuweza kupata matibabu bila gharama kubwa. Amesisisitiza kuwa bima ya afya itasaidia wananchi na familia zao kupata huduma bora za afya.