WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania imewasilisha miradi minane yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.334 katika Mkutano wa Nane wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaohusu ushirikiano wa Maendeleo baina ya Japan na Afrika (TICAD8) ambao umemalizika jana.
Miradi iliyowasilishwa ni ya ukarabati wa barabara ya Morogoro-Dodoma kwa kiwango cha lami, mradi wa umwagiliaji katika bonde la Ziwa Victoria, mradi wa kusambaza maji Lugoda (Mufindi), kujenga uwezo wa kituo cha utafiti cha ufugaji wa samaki Dar es Salaam, bandari ya kisasa ya uvuvi, kuanzisha maabara ya kuthibitisha ubora kwenye sekta ya uvuvi na ukarabati wa bandari ya uvuvi ya Wete na ujenzi wa njia ya umeme ya Somanga-Fungu-Mkuranga.
Akizungumza leo (Jumatatu, Agosti 29, 2022) jijini Tunis, Tunisia, ambako alikuwa akimwakilisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema alipata fursa ya kuwaeleza washiriki wa mkutano na nchi ya Japan juu ya utekelezaji wa miradi yake kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
“Kupitia mikutano ya TICAD, sisi tumenufaika na ujenzi wa daraja la Mfugale, mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi II, na sasa tumeomba watukamilishie miradi mitatu ya barabara ya Arusha-Holili, Bandari ya Kigoma na mradi wa maji wa Zanzibar,” amesema.
Miradi mitatu ambayo imeombewa fedha inahitaji kiasi cha dola za Marekani milioni 343.8 ambapo kati ya hizo dola za Marekani milioni 221 ni kwa ajili ya mradi wa barabara ya Arusha-Holili, dola milioni 98.7 (mradi wa kuboresha miundombinu ya usambazaji wa maji Zanzibar) na dola milioni 24.1 (bandari ya Kigoma).
Kuhusu sekta ya kilimo, Waziri Mkuu amesema kupitia TICAD8, Tanzania imeomba kupewa kipaumbele ili iweze kuongeza wigo wa kilimo. “Tunahitaji kuhakikisha tuna chakula kingi ili tuwe na ziada na tuweze kuuza nje ya nchi.
Waziri Mkuu pia alifanya mikutano na viongozi wa kampuni za Japan Tobacco Incorporation (JTI), Mitsubishi na Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA).
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa alimshukuru Mwenyekiti wa Bodi ya JTI, Bw. Mutsuo Iwai kwa kuamua kujenga shule ya bweni ya wasichana wilayani Urambo na akawaomba waendelee kununua zaidi tumbaki kutoka kwa wakulima.
“Mwaka jana walinunua tani milioni 14, kwa hiyo tumewaomba msimu huu waongeze tani zaidi ili kuwapa uhakika wa soko wakulima wetu. Wao wana kiwanda kwa hiyo wanaweza kununua zaidi,” amesema.
Pia, Waziri Mkuu alimshukuru Makamu wa Rais wa Kampuni ya Mitsubishi Bw. Yasuteru Hirai kwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya umeme mkoani Kilimanjaro na akaomba waangalie uwekezekano wa kuwekeza kwenye sekta ya kilimo na hasa kwenye uzalishaji wa mbolea.
“Eneo tunalolihitaji sana ni uzalishaji wa mbolea. Kama walivyofanya Asia kwa kuzalisha tani milioni 1.2, tumewaomba waje nchini kwa sababu mahitaji yetu ni makubwa. Pia tumewashawishi waje kujenga kiwanda cha kuunganisha magari hapa nchini badala ya kuagiza kutoka kwao.”
Naye, Rais wa JICA, Dkt. Akihiko Tanaka amemuahidi Waziri Mkuu kuwa wafanyakazi wa kujitolea waliokuwa wakifanya kazi nchini lakini wakalazimika kurudi Japan kwa sababu ya UVIKO-19 wataanza kurudi hivi karibuni ili waendelee kutoa huduma nchini.