Home Afya MAKAMU WA RAIS DKT. PHILIP MPANGO AHAMASISHA ELIMU YA AFYA KWA WANANCHI...

MAKAMU WA RAIS DKT. PHILIP MPANGO AHAMASISHA ELIMU YA AFYA KWA WANANCHI WA KIJIJI CHA KASUMO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesisitiza umuhimu wa wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kuwasaidia wananchi kwa kutoa elimu kuepukana na maradhi mbalimbali.

Makamu wa Rais ametoa wito huo mara baada ya kutembelea Zahanati ya Kijiji cha Kasumo akiwa wilayani Buhigwe mkoani Kigoma. Amesema maradhi yanayotajwa kuwasumbua wananchi wa Kijiji hicho ikiwemo magonjwa ya mfumo wa hewa pamoja na magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasio salama yanaweza kudhibitiwa kwa kutoa elimu kupitia mikutano mbalimbali ya Kijiji.

Amewahimiza wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuwatembelea wanakijiji katika maeneo yao na kuwaelimisha namna ya kuwalinda watoto dhidi ya michezo katika maji machafu pamoja na unywaji maji yasiochemshwa.

Amewataka wananchi wa Kijiji hicho kuweka utaratibu wa kuchemsha maji kabla ya kunywa na kuondokana na imani waliyonayo kwamba maji ya kuchemsha sio matamu.

Makamu wa Rais amewapongeza wanakijiji hao kwa kwa kujitoa katika kukamilisha zahanati hiyo ambayo imekua msaada kwa wananchi wa Kijiji hicho na vijiji Jirani.

Amewasihi wananchi wa Kijiji hicho kuendelea kujitolea na kushirikiana katika shughuli za maendeleo ili kuboresha Maisha yao kwa vizazi vya sasa na baadae. Aidha ametoa wito kwa wanakijiji hao kuanzisha nguvu mpya ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika zahanati hiyo.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekagua shuguli za maendeleo katika Wilaya ya Buhigwe ikiwemo ujenzi wa Shule ya Sekondari Kahimba pamoja na ujenzi wa barabara kiwango cha lami ya Muyama – Kasumo – Kabanga.

Amewataka wakandarasi kuhakikisha wanaongeza kasi katika ujenzi wa barabara hiyo wakati huu wa kiangazi ili ikamilike kwa wakati na kufungua shughuli za kiuchumi na kijamii katika Wilaya hiyo na maeneo Jirani.

Makamu wa Rais amesema serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itakamilisha miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa wa Kigoma ili kuvutia zaidi uwekezaji na kurahisisha shughuli za ufanyaji biashara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!