Na Boniface Gideon -TANGA
Kituo cha Sayansi jijini Tanga ‘STEM PARK’ kilichopo chini ya Project Inspire, mwishoni mwa wiki kimefunga mafunzo maalumu ya Teknolojia ya matumizi ya akili Bandia ( Akili Mnemba),kwa Wanafunzi Shule za msingi na Sekondari kutoka mikoa ya Tanga na Manyara.
Mratibu wa miradi kituo cha Sayansi Stem Park chini ya Project InSpire, Mashambo Kisakeni, amewaeleza Waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, wakati wa kuhitimisha wiki ya mafunzo waliokuwa wakiyatoa kwa wanafunzi wa mikoa ya Tanga na Manyara ambapo amesema kupitia miradi hiyo kumesaidia sii tu wanafunzi bali na walimu ambao wamepata mbinu mbalimbali za ufundishaji.
Aidha Mashambo ameongeza kuwa suala la maendeleo ya kiteknolojia katika ulimwengu wa kidigital wa sasa halikwepeki hivyo ni vyema wanafunzi wakajengewa uelewa mapema hatua ambayo itawasaidia kitaaluma na kuvitambua vipaji mbalimbali walivyonavyo.
Akizungumzia ushirikiano wa kituo cha Stem Park kilichopo chini ya Project InSpire na chuo kikuu cha Hong Kong,Mashamba
amesema lengo lao ni kuhakikisha wanazidi kuhamasisha juu ya matumizi ya Teknologia hususani kwa wanafunzi ili kuwajengea uwezo wao wa baadaye,
“lengo letu ni kuhakikisha Taifa linapata wataalamu wa baadae ambao watakuja kulisaidia Taifa letu katika Sekta mbalimbali,na tutaendelea kuwaandaa Wanafunzi kwa ngazi zote za Elimu, lakini tunaomba wazazi na walezi wawalete watoto wao hapa kituoni ili wapate Elimu ya teknolojia kwa vitendo” Alisisitiza Mashambo
Baadhi ya wanafunzi Akiwepo Anneth Kiumba na Arbogast Sandi wamepongeza kupatiwa elimu hiyo ambayo inazidi kuwapanua uwezo wao wa kiakili kutambua fursa mbalimbali za kiteknolojia katika sekta ya elimu,
“tunashukuru sana kwakupatiwa mafunzo haya, tulikuwa hatufahamu faida za roboti lakini kwasasa tumezifahamu,tunaweza kwenda kawapatia Elimu hii wenzetu lakini pia tunaomba iwe mwendelezo kwetu”Aliongeza Anneth
Mafunzo hayo yaliyodumu kwa muda wa wiki moja yakitekelezwa na Kituo Cha Stem Park chini ya Project Inspire kwa kushirikiana na chuo cha Hong Kong Politechnique University kilichopo nchini China yamewahusisha baadhi ya wanafunzi kutoka shule za msingi na Sekondari ikiwa ni mara ya pili kufanyika kwa mwaka huu wa 2024.