Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameyaomba makampuni ya gesi kutafuta namna ya kuwezesha kupatikana gesi kwa bei nafuu, ili wananchi wamudu bei ya bidhaa hiyo kwa matumizi ya kupikia.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 27 Juni 2024 alipofungua rasmi Bohari ya kwanza ya kuhifadhia Gesi ya Kampuni ya Oryx Gas Zanzibar Limited iliyopo Mangapwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ametoa rai kwa wananchi kuondokana na matumizi ya makaa na kuni hatua kwa hatua kwa ajili ya nishati ya kupikia, ili kupunguza athari za mazingira pamoja na kujiepusha na athari za kiafya zinazotokana na hewa sumu.
Rais Dkt. Mwinyi amepongeza uwekezaji wa Kampuni ya ORYX Gas Zanzibar Limited kwa kujenga matangi mawili yenye ujazo wa tani 1,388 sawa na kilo 1,388,000 za gesi.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi amesema kila mwananchi aliyehamishwa eneo la bandari jumuishi ya Mangapwani atalipwa fidia stahiki na makazi mbadala bila wasiwasi wowote.