Na Shomari Binda-Serengeti
MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Enock Mtambi, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Pongezi hizo amezitoa leo, Juni 28, kwenye kikao cha baraza maalum la madiwani kujibu hoja za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Akizungumza kwenye kikao hicho mara baada ya kupitiwa kwa hoja 63 zilizofanyiwa uchunguzi, amesema licha ya mapungufu ya kujibu hoja, Halmashauri imefanya vizuri kwenye ukusanyaji wa mapato.
Amesema katika kipindi cha miezi 6, Januari hadi Juni 2024, halmashauri hiyo imekusanya zaidi ya bilioni 4, kuvuka lengo la ukusanyaji wa zaidi ya bilioni 1, mapato ya ndani yanachangia uendeshaji wa halmashauri kwenye shughuli mbalimbali na amewapongeza madiwani kwa usimamizi mzuri.
“Niwapongezi kwa kazi nzuri ya usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kipindi hiki cha miezi 6 iliyopita, Lakini niwaombe madiwani kuwa na ushirikiano mzuri na watendaji kwenye kata zenu na sio kuwa na mivutano ili kuongeza ufanisi ikiwemo ukusanyaji wa mapato,” amesema.
Katika baraza hilo, Mkuu huyo wa Mkoa ametoa maagizo kwa madiwani ikiwa ni pamoja na kusimamia uongozi na kuhakikisha maazimio 5 ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali yanatekelezwa.
Amesema kupata hati ya ukaguzi yenye mashaka kunatokana na mafungu kwenye hesabu za mwisho na malipo ya wakandarasi, hivyo kuna haja ya kupata mafunzo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Serengeti, Ayubu Makuruma, amesema wamepokea maagizo ya Mkuu wa Mkoa ili kuondoa mashaka kwenye hati.
Amesema wanashukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi ambazo zimefanikisha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo.