Na Shomari Binda-Musoma
MADAKTARI bingwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wataanza kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwenye hospital ya manispaa ya Musoma kuanzia juni 24 hadi 28 mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Mganga mfawidhi wa hospital hiyo Dk. Emanuel Shani amesema kwa sasa wananchi wanaendelea kujiandikisha kwa ajili ya huduma hiyo.
Amesema shughuli ya uandikishaji inaendelea kufanyika hospitalini hapo ambapo matibabu yatazingatia uandikishaji uliofanyika.
Dk. Shani amesema fursa ya madaktari bingwa hao wa Rais Dkt. Samia inakuja kwenye hospitali ya manispaa ya Musoma hivyo wananchi wenye matatizo mbalimbali wanapaswa kuitumia.
Madaktari hao watatibu magonjwa ya kina mama, magonjwa ya watoto, upanuaji wa njia ya mfumo wa mkojo, magonjwa ya ndani, usingizi na ganzi, macho, mifupa pamoja na mionzi radioloji.
“Tunamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa madaktari bingwa kutufikia kwenye hospital yetu ya manispaa ya Musoma, kwa sasa tunawaomba wananchi wenye matatizo wafike hospitalini kwa ajili ya kujiandikisha kabla ya kuanza kutolewa kwa huduma juni 24”, amesema Dk. Shani
Baadhi ya wananchi waliofika hospitalini hapo kwa ajili ya kujiandikisha wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa huruma yake ya kuwaletea madaktari bingwa.
Wamesema wataitumia fursa hiyo kwa kuwa ni gharama kuwafuata kwenye hospitali kubwa kwa ajili ya kupata matibabu.