Na Mwandishi Wetu,
Wagonjwa zaidi ya 1,500 wamefanyiwa upasuaji na madaktari bingwa wa MOI katika hospitali ya Nyangao Mkoani Lindi katika kipindi cha miaka mitatu toka Taasisi ya MOI ilipoingia mkataba wa ushirikiano na hospitali hiyo ili kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini.
Kutokana na uwepo wa huduma za kibingwa za mifupa katika hospitali ya Nyangao, Serikali imeweza kuokoa zaidi ya Tsh Bilioni 2.7 ambazo zingetumika kusafirisha wagonjwa hao kufuata matibabu Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mh Shaibu Ndemanga ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mh Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wa mikoa ya kusini kwa kuwasogezea huduma za kibingwa za Mifupa na kuwaondolea adha ya kuzifuata huduma hizo MOI.
“Naomba nianze kwa kuishukuru Wizara ya Afya kwa kazi kubwa, Pia Kwanamna ya pekee naomba niishukuru Taasisi ya MOI ikiongozwa na Dkt. Respicious Boniface kwa kutekeleza kwa vitendo agizo la Serikali la kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi hususani katika mkoa wetu wa Lindi na kuwapunguzia gharama wananchi, jambo hili limewajengea imani kubwa wananchi kwa Serikali ” Alisema Mh. Ndemanga
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mtama, Bw. George Mbilinyi amesema uwepo wa huduma za kibingwa za mifupa za MOI katika hospitali ya Nyangao umepelekea wagonjwa kutoka mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma na mataifa jirani ya Msumbiji, Comoro na Malawi kufika hospitalini hapo ili kupata huduma.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt.Respicious Boniface amesema Taasisi ya MOI itaendelea kusogeza huduma zake karibu na wananchi ambapo hivi karibuni huduma za kibingwa za mifupa za MOI zitaanza kutolewa katika hospitali ya rufaa ya kanda ya kusini Mtwara .
“Tunashirikiana na wenzetu wa KCMC katika huduma za Ubongo na mishipa ya fahamu, tunashirikiana na wenzetu wa Bugando katika huduma za upasuaji wa magoti kwa njia ya Matundu, tunashirikiana na wenzetu wa Benjamin Mkapa katika upasuaji wa Nyonga na Magoti lengo letu ni kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi huko walipo kama Serikali inavyoelekeza” Alisema Dkt. Boniface.
Akitoa shukrani kwa niaba ya uongozi wa Hospitali ya Nyangao, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mtama Dkt. Dismas Masulubu ameishukuru Taasisi ya MOI kwa kuanzisha ushirikiano na Hospitali ya Nyangao ambapo wagonjwa wamekua wakipata huduma za kibingwa bila kulazimika kuzifuata huduma hizo Dar es Salaam.
Mwisho