Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amewaasa watumishi wote katika Sekta ya Maji kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni ili kufikia malengo ya kuwafikishia wananchi huduma toshelevu ya majisafi na salama.
Katibu Mkuu Sanga ametoa maelekezo hayo hivi karibuni kwa nyakati tofauti alipokutana na watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji katika Mikoa ya Katavi, Rukwa na Songwe.
“Sisi sote hapa ni watumishi wa umma; tunazo sheria, taratibu na kanuni za kiutumishi zinazotuongoza, ni muhimu kila mmojawetu akatimiza majukumu yake kwa kuzingatia haya mambo matatu,” alisisitiza Katibu Mkuu Sanga.
Mhandisi Sanga aliwaelekeza watumishi wote kwenye Sekta ya Maji kuepuka kuwa kero kwa wananchi na badala yake wawe ni wafumbuzi wa kero zinazowakabili wananchi hasa ikizingatiwa kwamba huduma ya maji haina mbadala na kwamba kila mwananchi anayo haki ya kupatiwa huduma bila kikwazo.
Aliwaasa watumishi hao kupenda kazi zao, kushirikiana, kuthaminiana, kupendana, kuheshimiana na kutambua jukumu la kila mmoja kwa jamii anayoihudumia ili kuepusha migongano isiyo ya lazima.
Alisema mwananchi anachohitaji ni kupata huduma ya maji haijalishi huduma hiyo anaipata kutoka kwenye Mamlaka ya Maji ama RUWASA na hivyo alizielekeza taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maji kushirikiana hasa ikizingatiwa jukumu la msingi la taasisi hizo ni kuhakikisha mwananchi anapata huduma toshelevu ya majisafi na salama.