Home Kitaifa DKT. NCHEMBA ALIOMBA BUNGE KUHIDHINISHIA WIZARA YAKE  BAJETI YA TRILIONI 44.19

DKT. NCHEMBA ALIOMBA BUNGE KUHIDHINISHIA WIZARA YAKE  BAJETI YA TRILIONI 44.19

Na Benny Mwaipaja, WF-Dodoma

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuiidhinishia Wizara yake makadirio ya mapato na matumizi ya kiasi cha shilingi trilioni 44.19, kati ya makadirio ya shilingi trilioni 49.35 za Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2024/2025, ili iweze kutekeleza vipaumbele vyake vitano ilivyopanga kuvitekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Ameeleza kuwa kati ya kiasi hicho kinachoombwa, shilingi trilioni 29.42 zitakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Misaada na mikopo inatarajiwa kuwa shilingi trilioni 5.13, mikopo ya kibiashara kutoka nje na ndani ya nchi inakadiriwa kuwa shilingi trilioni 9.60 na maduhuli ni shilingi bilioni 45.01.

kwa mwaka 2024/25, Wizara ya Fedha inaomba kuidhinishiwa matumizi ya jumla ya shilingi trilioni 18.17 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mafungu nane (8) ya kibajeti. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 17.63 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikijumuisha huduma ya deni la Serikali shilingi trilioni 13.13, mishahara shilingi bilioni 946.45, matumizi mengineyo shilingi bilioni 937.30 kwa mafungu ya wizara na taasisi zake, Huduma za Mfuko Mkuu shilingi trilioni 2.61 na matumizi ya maendeleo shilingi bilioni 544.05” Alisema Dkt. Nchemba

Aliliomba Bunge kuidhinisha pia bajeti ya Fungu 045 linalohusisha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi iidhinishiwe jumla ya shilingi bilioni 112.73 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 101.26 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 11.47 matumizi ya maendeleo. 

Alivitaja vipaumbele vitano vya mafungu ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/25 kuwa ni pamoja na kutafuta na kukusanya mapato ya shilingi trilioni 44.19 kati ya maoteo ya shilingi trilioni 49. 35 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya Serikali; Kuimarisha na kusimamia mifumo ya mapato, matumizi na mali za Serikali ikiwemo IDRAS, TANCIS, MUSE, NeST, CBMS na GAMIS; Kuhudumia deni la Serikali kwa wakati na kuboresha kanzidata ya kutunza taarifa za deni.

Dkt. Nchemba alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni Kutoa elimu ya huduma za fedha kwa wananchi kwa lengo la kukuza huduma jumuishi za fedha nchini; na Kujenga uwezo kwa wakaguzi wa ndani, kamati za ukaguzi pamoja na waratibu wa usimamizi wa vihatarishi katika taasisi za umma.

Mafungu 8 ya Wizara ya Fedha ni pamoja na Fungu 01- Deni la Serikali,  Fungu 06- Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali,  Fungu 10- Tume ya Pamoja ya Fedha, Fungu 13- Kitengo cha Kudhibiti Fedha haramu, Fungu 21- Hazina, Fungu 22- Huduma za Mfuko Mkuu, Fungu 23- Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali na Fungu 50- Wizara ya Fedha, huku Fungu 045 – linalosimamiwa na Wizara ya Fedga linalohusisha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi. 

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!