SERIKALI imetangaza kuajiri watumishi wa afya na walimu 16,676 kati ya nafasi za watumishi 17,412 wakiotakiwa huku nafasi 736 zilizokosa waombaji wenye sifa zikitarajiwa kutangazwa upya.
Haya yamebainishwa leo tarehe 26 Juni,2022 Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa wakati wa kutangaza ajira mpya za waalimu na kada ya afya zilizotangazwa Aprili 20, 2022.
Alisema jumla ya maombi 165,948 yalipokelewa kwenye mfumo ambapo maombi ya Kada za Afya ni 42,558, na Kada ya Ualimu ni 123,390.
Mhe. Bashungwa amesema kwa upande wa Kada za Afya, waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 6,876 wanawake ni 3,217 sawa na asilimia 46.8 na wanaume ni 3,659 sawa na asilimia 53.2 wakiwemo wenye ulemavu 42 sawa na asilimia 0.61 kutokana na uchache wa waombaji wenye sifa wa kundi hilo.
Amesema nafasi 736 kada za afya zilikosa waombaji wenye sifa ambazo ni Daktari wa Meno (50), Tabibu Meno (43), Tabibu Msaidizi (244), Mteknolojia Mionzi (86) na Muuguzi- ngazi ya cheti (313) na kusisitiza kuwa kada hizo zitarudiwa kutangazwa ili kupata waombaji wenye sifa watakaojaza nafasi hizo.
Bashungwa amesema kwa upande wa kada za ualimu, waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo na kupangiwa vituo vya kazi ni 9,800 ambapo walimu 5,000 wamepangwa shule za Msingi na walimu 4,800 shule za sekondari.
“Kati ya Walimu 5,000 wa shule za Msingi wanawake ni 2,353 sawa na asilimia 47.06 na wanaume ni 2,647 sawa na asilimia 52.94. Kwa upande wa walimu 4,800 wa Shule za sekondari wanawake ni 1,289 sawa na asilimia 26.85 na wanaume ni 3,511 sawa na asilimia 73.15.
Amesema pia walimu wenye ulemavu 261 wa shule za Msingi na Sekondari walioajiliwa ni sawa na asilimia 2.66 ya walimu wote walioajiliwa wakiwemo wanawake 84 na wanaume 177.
” Napenda ieleweke pia kuwa, kwa walimu wa sekondari tumetoa ajira za walimu wa sayansi kwa asilimia 76 ya nafasi 4,800 tulizopewa.”
Waziri Bashungwa ametaja vigezo vilivyotumika kuwa ni mwaka aliohitimu mtahiniwa kulingana na hitaji la kada au kiwango cha elimu, umri wa kuzaliwa waombaji wenye sifa waliopangwa na waombaji Wenye mahitaji maalum.
Aidha, Bashungwa amewataka waajiriwa wapya kuhakikisha wanaripoti kwa Wakurugenzi wa Halmashauri walizopangiwa wakiwa na kitambulisho cha taifa au namba ya utambulisho ya NIDA, Cheti halisi cha kuzaliwa, Vyeti Halisi vyote vya Taaluma na Utaalamu wa Kazi vya mwajiriwa, ili vihakikiwe na Mwajiri kabla ya kupewa barua ya ajira
Pia amewataka wajiriwa wapya ambao hawataripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya siku 14, tangu tangazo kutolewa, watakuwa wamepoteza nafasi zao na zitajazwa na waombaji wengine wenye sifa, waliopo kwenye Kanzidata (Database) ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI