Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Halmashauri zote nchini zihakikishe zinakamilisha uanzishwaji wa Madawati ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ifikapo Julai 2025.
Sambamba na hilo amesema, Halmashauri hizo pia zihakikishe masuala ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yanakuwa sehemu ya mipango na bajeti za kila mwaka, ili iwahudumie vijana wanaojishughulisha na masuala ya ubunifu, “kufanya haya kutasaidia kuimarisha uwezo wa nchi katika tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu”
Ametoa maagizo hayo leo (Ijumaa, Mei 31, 2024) katika Maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2024, yanayofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal jijini Tanga. Maadhimisho hayo ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuongeza hamasa ya kukuza elimu, ujuzi na matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais TAMISEMI zihakikishe kuwa ifikapo Julai 2025 Shule zote za Msingi, Sekondari, Vyuo vya Ualimu na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi viwe vimeanzisha Majukwaa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Awamu wa Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendeleza bunifu 283 zilizotokana na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU). “Tayari bunifu 42 kati ya hizo zimeshaingia Sokoni na imewezesha kuanzishwa kwa kampuni 94 kutokana na bunifu na teknolojia zinazobuniwa na wabunifu wa Kitanzania.”
“Nitoe wito kwa wabunifu nchini, mmebuni kazi na kazi hizo zinamatokeo, jipangni kuboresha kazi zenu, fungueni kampuni na mtangaze biadhaa hizo.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imeanzisha Vituo vya Umahiri 12 katika Taasisi za Elimu ya Juu na Taasisi za Utafiti na Maendeleo nchini. “Vituo hivyo vimeanzishwa kwa lengo la kuchagiza utafiti, ubunifu na ubiasharishaji wa matokeo yanayotokana na shughuli hizo”
Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuweka mfumo mzuri wa kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo pamoja na Mitaala iliyoboreshwa ili kuhakikisha kuwa malengo ya Serikali yanafikiwa.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kupitia miradi mbalimbali ya ujenzi miundombinu ya kutolea elimu katika ngazi zote za elimu nchini.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa jumla ya madarasa 4,043 yamejengwa kati ya hayo 3,992 ni ya shule za msingi na 51 ya sekondari, mabweni 109 pamoja na nyumba za walimu 253 zenye uwezo wa kuchukua watumishi 424.
“Sambamba na hilo, Serikali imewezesha ujenzi wa shule mpya za sekondari za kata 228, shule 26 za bweni za mikoa kwa ajili ya wasichana na shule mpya za msingi 302.”
Kwa Upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa Wizara hiyo inaendelea na hatua mbalimbali zinazolenga kuimarisha fursa na ubora wa elimu nchini kwa kutumia TEHAMA na teknolojia nyingine za kufundishia na kujifunzia.