Boniface Gideon, KILINDI
Waziri wa mambo ya ndani ya nchi mhamdisi Hamad Masauni ameagiza uchinguzi ufanyike kwa watu waliohusika na mauaji ya watu wawili yaliyotokea kijiji cha Lusane kata ya Tunguli wilayani Kilindi Mkoani Tanga.
Waziri Masauni ametoa agizo hilo Jana wakati alipofanya ziara wilayani humo katika hospitali ya Teule iliyopo mahali ambapo alikwenda akiwa ameambatana na uongozi wa Mkoa wa Tanga kwajili ya ukaguzi wa miili ya watu hao.
“Nimesikitishwa na tukio hili la kinyama dhidi ya raia wetu wa Tanzania jambo hili halikubaliki kwa namna yeyote ile sio utamaduni wetu na wala sio desturi yetu na hata katika mazingira ambayo wametendewa tukio hilo kama serikali tinataka tiwaeleze wananchi kwamba jambo hili tunalichukua kwa uzito unaostahili na titafanya kila linalowezekana kuhakikisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinawatia mkononi wahusika, “alisistiza Waziri Masauni.
Waziri Masauni amesema kwamba jambo hilo linaonyesha wazi dalili za uhalifu na kwamba kinachosubiriwa ni matokeo ya uchunguzi kwamba wahusika ni kina nani na wamefanya kwasababu gani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba amesema kuwa tukio hilo limeuchafua Mkoa wa Tanga huku akisema vyombo vya dola vitashirikiana kuwabaini wahusika wa tukio hilo.
Mgumba amesema dalili za awali zinaonyesha kuwa tukio hilo halijafanyika katika Mkoa wa Tanga na huku wamekuja kutupa kama jalalani ndio maana wameokotwa kwenye viroba.
“Watu wamewekwa kwenye viroba vya kilo 50 lakini wamekunjwa na kuonakana kama kilo 20, ni watu ambao wanaonekana wana uzoefu na kazi hii na wanaijua shghuli hii lakini kama alivyosema mheshimiwa Waziri vyombo vyetu viko kazini ili kuweza kuhakilisha wahalifu wa unyama huo wanakamatwa, “alisema Mgumba.
Alisema marehemu mmoja alikutwa akiwa amevaa nguo zaidi ya tano amevaa boksa, traksuti, suruali ya jeans, suruali ya kawaida, pensi ya jeans na suruali nyingine juu dalili zinazoashiria ni watu wanaojihusisha na biashara ya uchimbaji wa madini.
“Inaonekana watu hawa walikuwa na madini na baadae walikuja kubainika kwa wahalifu na hatimaye kutengeneza mpango wao lakini tuvipe nafasi vyombo vyetu vitatuthibitishia baadae serikali itakuja na kauli, “alibainisha RC Mgumba.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa Mgumba, amewataka watanzania kwa ambaye ndugu yake amepotea haonekani ndani ya Mkoa wa Tanga na hata nje ya Mkoa huo ili kuja kushuhudia na kuthibitisha kama ndio hao au watu wengine.
Viongozi mbalimbali walioshiriki kwenye ziara hiyo akiwemo Mbunge wa jimbo hilo Omari Kigua na Mkuu wa Wilaya hiyo Abel Busalama wamelaani vikali tukio hilo huku akiviomba vyombo vya dola kuwabaini wahusika wa tukio hilo.
Mbunge Kigua amesema kuwa tukio hilo linaweza kusababisha taharuki kwa watu wanaokwenda kuwekeza kwenye miradi ya madini na kwamba watu hao wanatakiwa wapatikane ili wawe mfano kwa watu wengine.
Naye Mkuu wa wilaya hiyo ametoa wito kwa wananchi wa eneo hilo kutoa taarifa pindi wanapoona gari ambayo hawaielewi au watu ambao wanawatilia mashaka kauli anayoitoa wakati wananchi wa eneo hilo wakidai waliiyona gari hiyo na hawakuitilia mashaka na mara baada ya kufuatilia wakakuta miili imetupwa.
Kwa upande wake Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga Safia Jongo amesema makao makuu ya polisi imeshaunda tume kwajili ya kushirikiana na polisi Mkoa ili kuwabaini wahusika wa tukio hilo.