Home Kitaifa NAIBU WAZIRI AKAGUA UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI SAME-MWANGA-KOROGWE.

NAIBU WAZIRI AKAGUA UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI SAME-MWANGA-KOROGWE.

Viongozi na wadau wa maendeleo mkoani Kilimanjaro wameipongeza serikali kwa jitihada za dhati katika kuhakikisha mradi wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe unakamilika, pongezi hizo zimetolewa wakati wa ziara ya kikazi katika mradi huo iliyofanywa na Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb).

Viongozi hao wa mkoa wa Kilimanjaro wamesema mradi huo umechelewa lakini sasa matumaini wanayaona kutokana na hatua zilizochukuliwa na serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Miongoni mwa viongozi hao ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga Mhe. Joseph Anania (Mb) ambaye amesema ametembelea mradi huo mara kadhaa lakini alikuwa hajapata mwanga wa maendeleo yake.

“Mhe. Naibu Waziri nimetembelea mradi huu mara kadhaa lakini sikuwa nimepata mwanga wa kutosha kuhusu utekelezaji. Kwa mfano nimepita kwenye hilo eneo linalotarajiwa kusimikwa pampu lakini sikuwahi kuoneshwa hizo pampu tatu zilizoletwa,kwa kweli niwapongeze sana kwa jitihada hizi kubwa zinazoendelea”alisema Mhe.Anania.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mwanga Jaffary Kandege amesema matumaini ni makubwa kwa wananchi wa Mwanga na kwamba hali halisi waliyoiona inatoa matumaini kwamba uwezekano wa kukamilisha mradi huo kwa haraka ni mkubwa, na kuipongeza serikali ya CCM.

Aidha, Mkurugenzi wa Kampuni ya M.A Kharafi & Sons ambaye ni mkandarasi amesema matumaini yao kwa sasa ni makubwa kutokana na nia ya dhati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakumba katika utekelezaji, amewahakikishia wakazi na wananchi wote wa Mwanga kuwa wasiwe na mashaka kwani vifaa muhimu kwa ajili ya kukamilisha mradi huo vimeshawasili na baadhi ambavyo havijafika wanatarajia kuvipokea bandarini mapema.

Naye Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amewataka viongozi wa Chama na Serikali kuhakikisha wanawapa wananchi taarifa sahihi kuhusiana na utekelezaji wa mradi huo,amesema kuna watu ambao wanatoa taarifa zisizo sahihi kuhusiana na mradi huo hivyo si vema wao viongozi wakakaa kimya.

Pia Mhe.Naibu Waziri amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatambua changamoto wanazopitia nwananchi wa Same Mwanga na Korogwe na kwamba anafanya kila jitihada kuhakikisha mradi huo unakamilika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!