Na Scolastica Msewa, Kibaha
Wakala wa Vipimo Tanzania WMA wamesema wapo tayari kutoa ushirikiano kwa wananchi wenye mashaka au changamoto yoyote ya Vipimo kwa lengo la kujiletea maendeleo.
Hayo yamesemwa na Meneja wa wakala wa Vipimo Tanzania WMA mkoa wa kihuduma Misugusugu Charles Mavunde wakati wa maadhimisho ya siku ya Vipimo duniani katika viwanja vya Misugusugu Kibaha mkoani Pwani.
Alisema Wakala wa Vipimo Tanzania wapo tayari kutoa ushirikiano kwa wananchi wenye mashaka au changamoto ya dira za maji, mizani ya maduka, mita za umeme, matanki ya magari yabebayo vimiminika ili kutoa huduma na kuuza bidhaa zenye ujazo, uzito na urefu unaoenda na thamani ya fedha ya mteja.
“Waje wakiwa na changamoto yoyote hata kama wakitaka ushauri wa aina yoyote na changamoto yoyote inayohusu masuala ya Vipimo tutashirikiana nao na ndio kazi yetu wakala wa Vipimo Tanzania” alisema Mavunde.
Aidha Mavunde aliwataka Waandishi wa Habari kuendelea kutoa ushirikiano wa kuelimisha jamii kuhusu jamii kuhusu Wakala wa Vipimo ilikumletea mwananchi maendeleo kama kauli mbiu ya mwaka huu ya Maadhimisho ya siku ya Vipimo duniani inayosema “Tunapima leo kwa kesho endelevu“
“Hii ni hatua ya kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020 ambayo inataka katika sekta ya maji inataka kufikisha huduma kwa jamii kwa mijini asilimia 95 na asilimia 85 vijijini ifikapo mwaka 2025 pia kuboresha huduma za umeme mijini na vijijini kupitia REA na kuboresha Nishati ya mafuta na gasi” alisema Mavunde.
“Waandishi wa Habari tushirikiane katika kutekeleza Ilani na kusogeza huduma kwa wananchi kwa maendeleo endelevu ya nchi” alisema Mavunde.
Aidha katika maadhimisho hayo Wakala wa Vipimo Misugusugu wametoa tuzo na vyeti vya pongezi kuwa Wadau Wazuri wanaotoa ushirikiano kwa Wakala hao ambapo alizitaka taasisi hizo kuwa ni pamoja na makampuni ya nishati na gasi, idara za maji na Wadau wake ikiwemo DAWASA, TANESCO na Wadau wanahusika na usambazaji, ufungaji wa bidhaa zenye kupimwa katika jamii.
“Lengo likiwa ni kuhamasisha mwananchi anahudumiwa vizuri ilikupata maendeleo endelevu katika taifa letu” alisema Mavunde.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Misugusugu Upendo Ngonyani ambaye alikuwa Mgeni rasmi amewataka Wadau wa vyombo vya usafirishaji wa vimiminika kusaidia serikali kupima matanki ya magari yabebayo vimiminika ilikutoa Vipimo sahihi kwa wananchi.
Aidha waliwapongeza Wakala wa Vipimo kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM hususani katika kuhakiki mizani, dira za maji, mita za umeme.
Hatahivyo aliahidi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhakiki mizani, dira za maji na Miata za umeme.