Na. Saidina Msangi, WF, Dodoma.
Serikali imesema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) haitozi kodi kwa wasafiri kati ya Zanzibar na Tanzania bara wanaobeba vitu kwa matumizi binafsi.
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Danie Silo (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Konde, Mhe. Mohamed Said Issa, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itawaondolea usumbufu wa kikodi wananchi wanaobeba vitu vya matumizi binafsi wanaposafiri kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.
‘‘Changamoto hujitokeza wakati wafanyabiashara wengine wasiokuwa waaminifu kubeba vitu vya biashara na kutokutaka vitozwe kodi, Wafanyabiashara hao wanavipitisha bandarini wakiwa wamevigawanya kwa abiria au kutumia wabeba mizigo wa hapo bandarini ili kuvitoa’’, alifafanua Mhe. Silo.
Mhe. Silo alisema kuwa baada ya bidhaa hizo kupita maeneo ya bandari mfanyabiashara husika anakabidhiwa vitu vyake bila kuvilipia kodi ambapo kutokana na utaalamu na weledi wa maofisa wa forodha mazingira kama haya ya wafanyabiashara hao hugundulika.
Mhe. Silo aliongeza kuwa mchezo huo ukigundulika wafanyabiashara hutelekeza mizigo hiyo bandarini na kuanza kutoa lawama kwa TRA kwamba wanashikilia bidhaa za wasafiri kitu ambacho hakina ukweli wowote.