WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi wawe wavumilivu hadi msimu wa mvua uishe ndipo Serikali itafanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu na kujua mahitaji halisi.
“Tumepata mafuriko katika maeneo mengi Nchini. Mtuvumilie, tusubiri hali ya mvua iishe. Tunachelea kuweka hela ya ujenzi halafu mvua ije inyeshe na kusomba tena miundombinu. Endeleeni kuwa na matumaini na Serikali yenu, endeleeni kumwamini Rais wetu,” amesema.
Ametumia fursa hiyo kuwafikishia wana Kyela salamu za pole kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hutokana na mafuriko yaliyotokea wilayani kwao tangu mwezi Aprili, 2024.
Ametoa wito huo leo (Jumapili, Mei 12, 2024) wakati akizungumza na wananchi na wadau wa zao la kakao waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Chama Kikuu cha Ushirika cha Kyela (KYECU) mara baada ya kukagua ghala la kakao la chama hicho.
Amewataka wakulima wa zao hilo waendelee kuhakikisha mashamba yao yanakuwa masafi ili kuzuia magonjwa na wadudu waharibifu. “Mashamba yenu hayana magugu ndiyo sababu mazao yenu hayana magonjwa. Endeleeni kusafisha mashamba ili kuzuia wadudu wanaoweza kuharibu zao hili.”
Naye, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema wizara hiyo ina nia ya kuzalisha miche mingi ya mbegu ili iweze kugawiwa bure kwa wakulima. “Tumeomba tupatiwe eneo ili tuzalishe zaidi miche ya mbegu bora hadi kufikia 100,000 kutoka 34,000 ya sasa.”
Alisema wizara hiyo pia inao mradi wa umwagiliaji wa sh. bilioni 21 ambao unajengwa wilayani Kyela na utahudumia vijiji saba vikiwemo vya Makare, Mababu na Ilovo.
Akielezea kuhusu ukungu unaosumbua zao la kakao, Naibu Waziri huyo amesema zao hilo bado ni organic kwa hiyo linahitaji dawa ambazo si za viwandani. “Nimewaagiza TARI waje wafuatilie na kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.”
Mapema, akiwa katika kijiji cha Kilombero katika kata ya Mababu, wilayani Kyela, Waziri Mkuu alikagua shamba la mkulima wa kakao, Mzee Clement Msalangi lenye ukubwa wa ekari sita.
Mzee Msalangi alimweleza Waziri Mkuu kwamba shamba hilo lenye miche zaidi ya 4,000 linampatia mavuno ya tani tatu za kakao kwa mwaka. Bei ya kilo moja kwa sasa ipo kati ya sh. 25,000 na sh. 32,000.
Awali, akitoa maelezo kuhusu zao hilo mbele ya Waziri Mkuu, Afisa Kilimo wa Kata hiyo, Benjamin Mwaijumba alisema wakulima wa kata hiyo wanalima aina mbili ambazo ni Criollo na Forastero ambazo zote zina bei moja lakini zinatofautiana kwenye uzalishaji.
“Forastero inazaa zaidi kuliko Criollo na wakulima wengi wa Kyela wanalima aina ya Forastero,” alisema na kuongeza kuwa kakao haina msimu akimaanisha kuwa ikifikisha miaka minne hadi mitano, mkulima akianza kuvuna, ni mwaka mzima.