SERIKALI imeanza mchakato wa ujenzi wa kituo jumuishi cha huduma za parachichi ambacho kitasaidia kuhifadhi na kuchakata zao la Parachichi kitakachojengwa eneo la Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.
Akizungumza baada ya Waziri Mkuu Kassim majaliwa ambaye yuko ziarani Mkoani Mbeya kuhoji kuhusu changamoto ya kuharibika kwa parachichi za wakulima katika eneo hilo, Mkurugenzi wa Mazao kutoka Wizara ya Kilimo Enock Nyasebwa amesema kuwa wako katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za kimkataba ili kumuwezesha mkandarasi kuanza ujenzi.
Ameyasema hayo jana (Jumamosi Mei 11, 2024) katika mkutano wa hazara wa Waziri Mkuu uliofanyika Kiwira wilayani Rungwe mkoani Mbeya.
“Ujenzi wa kiwanda hiki utawezesha kuongeza thamani ya zao la parachichi kwani itawezesha wakulima kuhifadhi mazao yao katika chumba baridi pamoja na kuchakata mazao yatokanayo na matunda hayo ikiwemo mafuta“.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa katika kuhakikisha wanaongeza zaidi thamani ya zao hilo, wameanza mpqngo wa kuweka vugezo ili kuhakikiwha miche inayopandwa inakiadhi vigezo lengo likiwa ni kupata zao lenye ubora ambayo litafanya vizuri kwenye soko la kimataifa ili kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi huyo kuhakikisha wanakamilisha taratibu zilizobaki ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu kilimo bora cha zao la parachichi ili kuongeza thamani na ubora.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Busokelo lililoko eneo la Lwangwa na kuweka jiwe la msingi kwenye jengo hilo.
Mapema, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Busokelo, Bi. Loema Peter alimweleza Waziri Mkuu kwamba ujenzi wake umefikia asilimia 94 na akaomba Serikali ikamilishe taratibu za upatikanaji wa sh. bilioni 2.3 ili waweze kukamilisha hatua iliyobakia.
Alisema hadi hadi sasa wamekwishapokea shilingi bilioni 6.08 za ujenzi na shilingi milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa samani za ofisi hizo.