Na Cleopatra Mgonja, Dar es Salaam
April 6 2024 Tanzania ilipata nafasi ya kuwa mwenyeji wa kongamano Womelifthealth Global uliohudhuriwa na nchi 41 ulimwenguni.
Kongamano hilo la siku tatu uliobeba ujumbe usemayo “Kufikiria upya njia mpya za uongozi kwa changamoto mpya ni kuleta pamoja akili angavu zaidi duniani ili kuhamasisha hatua za pamoja za kutumia nguvu za wanawake kwa ajili ya kuboresha watu wote”
Mkutano huo wa kimataifa uliofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) uliop jijini Dar es salaam mgeni rasmi alikuwa makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Dr Philip Mpango ambaye alifungua mkutano huo kwa kusema kuwa ni muhimu kushughulikia changamoto mbalimbali kama vile mila potofu na mabadiliko ya tabianchi ambazo ni kikwazo kwa wanawake kufikia nafasi za juu za uongozi katika sekta ya afya na nyinginezo.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa WomenLift Health 2024 unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Amesema kuendelea kufuata mila potofu kama vile ukatili na ndoa za utotoni ni kikwazo kwa wanawake kufikia uongozi wa juu. Ameongeza kwamba Tanzania ambayo ina makabila 123 kwa kiasi kikubwa yamekuwa na mfumo dume ambao huwalazimisha wanawake kutunza familia zaidi kuliko kujiendeleza kitaaluma na kiuongozi.
Pia ametoa wito wa kuelekeza rasilimali za kifedha zaidi ili kuwajengea uwezo viongozi wanawake na kujenga ufahamu kuhusu uwezo wao katika jamii. Amesema bado maeneo hayo yameendelea kupewa kipaumbele cha chini katika bajeti na hivyo kushindwa kuwajengea uwezo wanawake viongozi kama vile wabunge, wachambuzi wa sera na watafiti.
Makamu wa Rais amesema katika uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hatua mbalimbali zimechukuliwa katika kuhakikisha wanawake wanashiriki katika uongozi na kutumia vipaji vyao katika kukabiliana na changamoto za sekta ya afya. Aidha ametaja maeneo ambayo serikali imewekeza kuwawezesha wanawake kama vile ujenzi wa shule maalum za sayansi kwa wanawake, uteuzi wa nafasi mbalimbali za uongozi, kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya sayani kupitia Samia Scholarship Program pamoja na programu ya kuwarejesha wasichana shule waliokabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile kupata ujauzito na umasikini.
Pia Makamu wa Rais amesema serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama ili kusaidia wanawake hususani maeneo ya vijijini kutumia muda mwingi kutafuta huduma hiyo, kuongeza nishati safi ya kupikia, kuanzisha program maalum ya kumsaidia mama mjamzito kujifungua salama ya M- Mama, pamoja na kutekeleza lengo namba 3 la Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa kupunguza vifo vya mama na mtoto kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015 hadi vifo 104 kwa kila vizazi 100,000 mwaka 2022.
Mh. Dkt Philip Mpango alifikisha salamu kitoka kwa Mh Dr Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wote waliohudhuria mkutano huo na kuwasahii wasiache kutembelea vivutio vya utalii vya Tanzania bara pamoja na Zanzibar.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema ajenda za mkutano huo ambazo ni pamoja na uongozi wa mabadiliko, kuchukua hatua katika kuongeza wanawake kwenye nafasi za juu za uongozi katika sekta ya afya na ushirikiano kama njia ya usawa wa kijinsia zinaenda sambamba na vipaumbele vya serikali ya awamu ya sita inayolenga mabadiliko, maridhiano, ujenzi mpya, ustahimilivu na mageuzi.
Aidha Waziri Ummy amesema chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Sekta ya afya imepiga hatua kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, magonjwa yanayoambukiza, afya ya mama na mtoto pamoja na kuendelea jitihada za kuhakikisha inapatikana bima ya afya kwa wote.
Awali akitoa taarifa ya Mkutano huo Rais wa WomenLift Health Bi. Amie Batson amesema pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wanawake ya asilimia 70 ya watumishi katika sekta ya Afya Duniani bado changamoto ni idadi ndogo ya wanawake katika uongozi wa juu kwenye masuala ya afya. Amesema kutokuwepo kwa usawa katika uongozi wa juu kwenye sekta ya afya kunakwamisha namna ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta hiyo.
Rais mstaafu Dr Jakaya Mrisho Kikwete pia alihudhuria na kushiriki katika safu ya wasemaji ikijumuisha Gumzo la Fireside lililomshirikisha Rt. Mhe. Helen Clark, Waziri Mkuu wa zamani wa New Zealand mazungumzo hayo yalielezea uharaka wa kuweka usawa wa kijinsia katika jibu la ulimwengu kwa matishio yanayoibuka ya kiafya, na kwa kutumia uzoefu na maarifa tele na nini kifanyike ili kuchochea hatua za pamoja ili hatimaye kuwainua viongozi wanawake kwa manufaa ya ubinadamu wote.
Kongamano la Women lift health lilibeba agenda nyingi za jinsi gani ya kumkomboa mwanamke na jamii kutambua nafasi ya wanamke sambamba na mada kuu zikiwa kwanza kabisa ni Uongozi Unaobadilika Pili, Ushirika kama Njia ya Usawa wa Jinsia Mwisho Hatua ni Kuendeleza Uongozi wa Wanawake katika Afya.