Home Kitaifa MWENEZI MKOA WA PWANI KUMSAKA MTENDAJI ALIYE KULA MIL. 8

MWENEZI MKOA WA PWANI KUMSAKA MTENDAJI ALIYE KULA MIL. 8

KATIBU wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani David Mramba ameapa kulivalia njuga suala la Mtendaji ambaye anadaiwa kupokea kiasi cha Mil.8 ili kuziba barabara iliyoharibika malalamiko ambayo yamewasilishwa na Katibu Siasa na Uenezi Kata Kibaha Vijijini Pendo Ernest.

Mramba amesema hayo Mlandizi wilayani kibaha mkoani Pwani wakati akitoa mada kwa Makatibu wa Siasa, uenezi na mafunzo wa kata ya kibaha vijijini ambapo Endo amedai kuwa fedha hizo alikabidhiwa aliyekuwa Mtendaji wao (hakumtaja jina) ambaye hivi sasa amehamishiwa Kata ya Dutumi.

“Tunajua kwamba pesa ilitolewa na Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini kiasi cha Mil.nane lakini kifusi kilichowekwa ni kidogo hivyo kimezalisha tope ambalo hata magari yanashindwa kupita kutokana na barabara kuzidi kuwa mbovu” amesema.

“Changamoto iliyojitokeza ni kuharibika kwa kipande cha barabara hali iliyopelekea Mhe. Mbunge wa Kibaha Vijijini kutoa Mil.nane ili kuwekwe kifusi lakini hakikuwekwa tumemuuliza Mhe.Diwani ametujibu kuwa pesa bado ipo lakini hakuna utekelezaji wowote” ameongeza.

Katibu wa CCM Tawi la Mkwajuni Kata ya Mtambani Kibaha Vijijini Khadija Ameir Maguto amemueleza Mramba kuwa wananchi wake wanahitaji utekelezaji wa barabara ya Makofia Mzenga Bagamoyo.

“Sisi viongozi tunapata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi zoezi la ujenzi limeanza miaka mingi lakini hakuna utekelezaji tuliambiwa kuwa Desemba mwaka 2023 tutalipwa lakini hadi sasa hakuna utekelezaji”

Hayo yamejiri leo Aprili 24 katika ziara ya Mwenezi Mramba aliyoipa jina la Ste By Step katika Tarafa ya Mlandizi, Wilaya ya Kibaha vijijini iliyofanyika katika Ukumbi wa Pentagon uliopo karibu na Stendi Kuu ya magari Mlandizi.

Aidha katika ziara hiyo, Mwenezi wa Mkoa wa Pwani David Mramba ametoa mafunzo mbalimbali kwa Makatibu wa CCM na Wenezi wa Matawi, Makatibu wa CCM na Wenezi wa Kata za Tarafa hiyo na Makatibu wa Hamasa wa Kata hizo.

Aidha mafunzo mengine yaliyotolewa ni suala zima la Itifaki ya ukaaji, Itifaki ya bendera, Itifaki ya magari na Itifaki ya Mavazi, Uongozi na Maadili elimu iliyotolewa na Katibu wa Vijana Kibaha Vijijini Jacob Kituu.

Aidha Mramba amewasisitiza wanachama kuendelea kuheshimiana, kuthaminiana, na kusaidiana ili kufikia malengo ya Chama CCM

Amesema ni wajibu wa kila mwanachama kulipa ada na kujitoa ndani ya chama huku akiwataka kutimiza majukumu yao kutokana na Katiba ya CCM inavyoeleza.

Amewataka wanachama wa CCM Kibaha Vijijini kuwa wamoja ili waweze kukijenga chama na kujiandaa na mikakati madhubuti katika kuelekea chaguzi zilizopo mbele yao ambazo ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji, Vitongoji, na 2025 uchaguzi Mkuu.

Amewakumbusha kuwa nafasi walizo nazo ni dhamana hivyo wanatakiwa kuzitumia kwa maslahi ya Chama na si kwa maslahi
yao binafsi.

Aidha amewakemea baadhi ya wanachama kuanza kuandaa wagombea kabla ya muda wa uchaguzi jambo ambalo linatengeneza makundi na kukigawa chama.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!