Home Kitaifa UCSAF YATAKIWA KUSIMAMIA KWA KARIBU UJENZI WA MINARA YA MAWASILIANO

UCSAF YATAKIWA KUSIMAMIA KWA KARIBU UJENZI WA MINARA YA MAWASILIANO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa maagizo kwa Taasisi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuendelea kusimamia kwa karibu ujenzi wa minara ya mawasiliano na kuhakikisha vijiji ambavyo havina huduma za uhakika za mawasiliano ya simu vinapata mawasiliano.

Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo wakati wa uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Ofisi ya Taasisi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) lililopo eneo la Njedengwa mkoani Dodoma. Amesema ni muhimu kuhakikisha Wananchi wanapata mawasiliano ya uhakika wakati wote ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi hususan katika kipindi hiki ambapo huduma nyingi zinawezeshwa na huduma za mawasiliano.

Aidha Makamu wa Rais ameitaka UCSAF kuendelea kutekeleza miradi ya kuongeza uwezo wa minara kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G.  Amesema huduma nyingi za jamii hivi sasa zinawezeshwa kwa kutumia intaneti ni muhimu kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma hiyo mijini na vijijini.

Vilevile Makamu wa Rais ameiagiza UCSAF kujipanga kuongeza misaada ya vifaa vya TEHAMA hususan kwenye shule za umma ili kuongeza hamasa kwa wanafunzi kupenda masomo ya TEHAMA na kukuza matumizi ya intaneti nchini. Ametoa  wito kwa sekta binafsi na sekta ya umma kushirikiana na UCSAF kuongeza idadi ya shule zinazopokea huduma hiyo na vifaa vya TEHAMA ili kuwezesha watoto kujifunza kwa urahisi.

Halikadhalika ametoa wito kwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kushirikiana na wadau ikiwemo sekta binafsi kuona uwezekano wa kuiongezea UCSAF uwezo, ikiwemo fedha na rasilimali nyingine ili kuiwezesha kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yasiyo na huduma ya televisheni na redio za hapa nchini. Amesema ni vema  UCSAF iangalie uwezekano wa kuwezesha matangazo ya televisheni na redio kuwafikia wananchi kwa njia ya mtandao.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema kupitia UCSAF asilimia 98 ya wananchi waliopo katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mjini yasio na mvuto wa kibiashara wamenufaika na huduma za mawasiliano. Ameongeza kwamba wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini wamepata fursa ya kushiriki katika mageuzi ya kidijiti nchini kwa kuwa sehemu ya watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya mtandao.

Aidha Waziri Nape amesema sekta ya mawasiliano imeendelea kukua kwa kasi hapa nchini ambapo kufikia mwaka 2024 jumla ya laini za simu milioni 72 zimesajiliwa kulinganisha na laini za simu milioni 51 mwaka 2020. Pia amesema zaidi ya minara 600 hapa nchini inatumia huduma ya 5G.

Amesema kwa sasa ni muhimu kufanya uwekezaji wa namna ya kutengeneza vifaa vinavyotumia mtandao ikiwemo simu janja hapa nchini ili uwekezaji unaofanywa na serikali katika kuboresha mawasiliano kuendelea kuwa na tija.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Mngereza Mzee Miraji amesema kupitia UCSAF kwa kipindi kifupi jumla ya minara 47 imejengwa Zanzibar pamoja na ujenzi wa vituo 11 vya tehama Unguja na Pemba ambavyo imekua vikisaidia vijana kwa kiasi kikubwa.

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ni Taasisi ya Serikali ambayo ina jukumu la kuhakikisha mawasiliano yanafikishwa katika maeneo ya vijijini na mjini yasio na mvuto wa kibishara. Mfuko huo hushirikiana na watoa huduma za mawasiliano katika kujenga minara inayowezesha upatikanaji wa mawasiliano ya simu pamoja na uimarishaji wa matangazo ya redio na televisheni.

Uzinduzi wa Jengo hilo ni shamrashamra kuelekea Miaka 60 ya Muungano.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!