Balazi wa Norway nchini Tanzania Tine Tonnes amesema Serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza sekta ya kilimo ili kuwawezesha wakulima hapa nchini kuweza kunufaika na kilimo kwa kuwapatia masoko na teknolojia za kisasa ambazo zitawawezesha kuzalisha kwa tija.
Balazo huyo ameyasema hayo wakati akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima walipokutana wakijadili namna gani sekta ya kilimo inaweza kukuza uchumi wa wakulima katika Mkoa huo.
Amesema kwa sasa asilimia kubwa ya mazao ya kilimo yanayozalishwa hapa nchini yanaweza kushindana katika soko la kimataifa na hii inatokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuwapatia teknolojia za kisasa katika ufanyaji wa shughuli za kilimo hapa nchini.
Amesema ili kilimo kiweze kuwa na tija katika nchi yeyote ile ni lazima wakulima wake waweze kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji wa mazao,hivyo kutokana na ushirikiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya mataifa hayo mawili Serikali ya Norway itaendelea kushirikiana na Tanzania juu ya ukuzaji wa sekta ya kilimo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema kwa sasa Serikali ya Mkoa huo imejikita katika kuendeleza mazao ya kimkakati ambayo yatasaidia kukuza uchumi wa Mkoa na mkulima mmoja mmoja katika Mkoa huo.
Amesema mazao ambayo kwa sasa yanapewa kipaumbele katika Mkoa huo ni pamoja na  zao la parachichi, kakao, mazao yote ya viungo na zao la mchikichi ambapo ameongeza kuwa endapo mazao hayo yataweza  kulimwa kwa wingi basi asilimia kubwa ya wakulima wanaweza kuondokana na wimbi la umasikini.
Naye Mkurugenzi wa  Mtendaji wa Taasisi ya kuendeleza kilimo katika ushoroba za Kilimo Tanzania Geofrey Kilenga amesema katika ziara hiyo balozi ametembelea baadhi ya  wakulima waliopo katika safu za milima ya Urugulu na kujionea namna gani wanavyozalisha mazao ya viungo.