NA.MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu ameeleza hadi sasa maandalizi ya zoezi la Sensa ya Watu na Makazi nchini yamefikia zaidi ya asilimia 95 huku akihimiza wananchi kuwa tayari kuhesabiwa ifikapo tarehe 23 Agosti, 2022.
Ameyasema hayo wakati akiongoza kikao cha saba cha Kamati ya Ushauri ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kilicholenga kumepokea taarifa ya hali ya maandalizi kuelekea Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yenye kauli mbiu isemayo “Sensa kwa Maendeleo, Jiandae Kuhesabiwa”
Dkt. Jingu alitumia jukwaa hilo kuwaasa wananchi wote kuwa tayari kuhesabiwa kwa kuzingatia umuhimu wa zoezi la sensa katika kujiletea maendeleo nchini hususani katika kuchagiza mipango ya Taifa inayoendana na idadi ya wananchi waliopo.
“Ni wajibu wa kila mtu kuona umuhimu wa zoezi hili na kuwa tayari kuhesabiwa kwa kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa wakati unapofika ili malengo ya zoezi hili yafanikiwe kama ilivyopangwa,”alieleza Dkt. Jingu.
Aidha kamati hii inafanya kazi chini ya uongozi wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi inayoongozwa na Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar namna bora ya utekelezaji wa Sensa ili kufikia malengo yaliyopo.
Akifunga kikao hicho, mwenyekiti mwenza wa Kamati hiyo ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar Bw.Salhina Ameir alipongeza hatua ya maandalizi iliyofikiwa huku akihimizai kila mmoja katika eneo lake kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha zoezi la sensa linafanikiwa kwa utulivu na amani.
“Ni kazi kubwa imefanyika, nawapongeza sana na tunatambua mchango wa kila mmoja wenu katika nafasi yake katika kuhakikisha tunafikia malengo kwa ushindi mkubwa nitoe rai tuendelee kushirikiana kwa lengo la kuleta matokeo chanya,”alisema Ameir