Serikali za Tanzania na Zambia zimefanikiwa kufuta kero nne kati ya kero 15 zilizokuwepo awali ili kurahisisha michakato ya biashara ya nchi hizo kutegemeana kibiashara.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Zanzibar, Mhe. Omar Shaaban wakati wa Mkutano wa tatu (3) wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya Tanzania na Zambia ngazi ya Mwaziri uliofanyika Tunduma-Tanzania Aprili 18, 2024.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Shaaban amesema kuwa kikao hicho ni utekelezaji wa maelekezo ya Wakuu wa nchi zote mbili Tanzania na Zambia ambao walikutana jijijni Lusaka mwezi Oktoba, 2023 ambapo miongoni mwa makubaliano ni pamoja na Mawaziri wa pande mbili wanaohusika wakae na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara katika nchi hizo.
“Tuliingia katika majadiliano haya tukiwa na changamoto 15 na ndani ya siku tatu hizi tumeweza kutatua kabisa changamoto nne na katika hizo nne mbili zilikuwa upande wa Zambia na mbili zilikuwa Tanzania.Jambo la msingi wenzetu wa Zambia walikuwa wanashindwa ‘ku-process’ mizigo kwa haraka pale boda changamoto kubwa walikuwa hawana ‘scanner’, tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa ‘scanner’ kwa ajili yao. Na ilichukua muda mrefu kupokea lakini tunafuraha juzi wameandika barua kuwa wameipokea na wako tayari kwenda kuifunga” Amesema Mhe Shaaban
Ameeleza kuwa Zambia kulikuwa na vizuizi vingi kutoka mpakani hadi kufika jijini Lusaka ambapo sasa vimepunguzwa kutoka 33 vilivyokuwepo awali mpaka 11.
“Kwa kweli ni hatua kubwa wenzetu wa Zambia wameweza kurahisisha mazingira ya biashara ndani ya nchi zetu. Kubwa lingine sio changamoto ya kibiashara ni maelekezo ya Wakuu wetu kuhakikisha tunaanzisha mchakato wa kutengeneza boda nyingine kule Kasesya ambayo itaunganisha nchi zetu hizi mbili ni hatua kubwa na kikao hiki kimethibitisha kwamba tayari timu imeshaandaliwa michakato kuanza” Amebainisha.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Zambia, Mhe. Chipoka Mulenga amesema kuwa changamoto zilizotauliwa zina maslahi kwa nchi zote mbili.
“Tumetatua baadhi ya changamoto zilizokuwa na maslahi kwa nchi zetu zote mbili Tanzania na Zambia kurahisisha ufanyikaji wa biashara ikiwa ni kuongeza wafanyakazi, na kutoa vizuizi vingi njiani ambavyo vilikuwa vinasababisha foleni”
Tumetatua changamoto ya ‘scana’ ambayo kutokana na mahusiano ya kidiplomasia tumepewa scanakutoka Tanzania. Tunaamini changamoto zilizobaki mawaziri wetu wakikutana watatatua zaidi kwa maslahi mapana ya nchi zetu ili kurahisisha ufanyikaji wa biashara” Amesisistiza.