Na Magrethy Katengu
Benki ya Akiba (ACB) imezindua rasmi huduma ya kadi za VISA ambazo ni mahususi kwa kufanya huduma za miamala ya kifedha ambapo ina uwezo wa kutumika sehemu yoyote Duniani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo wa ACB VISA, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Silvest Arumasi amesema kwamba Benki ya ACB inafanya maboresho makubwa ya huduma za kifedha kwa wateja wake ili kuendana na mahitaji ya soko.
Aidha amesema kwamba maboreshao hayo yatasaidia kukidhi matarajio ya wateja ambapo hivi sasa huduma nyingi za kibenki zinatolewa kidigitali nakusaidia wateja kupata huduma kwa haraka na rahisi zaidi.
“Huduma za ACB VISA CARD zinamrahisishia mteja kufanya miamala mbalimbali kidigitali mfano kutoa pesa kwenye ATM mbalimbali za VISA popote Duniani na kufanya manunuzi mtandaoni, kufanya malipo kwenye vituo vya mafuta, kwenye migahawa na kwenye maduka makubwa (Shopping malls & supermarkets) na nyingine nyingi” amesema Silvest
Bw. Silvest amewashukuru wateja wote kwa kuendelea kuiamini ACB na kufanya biashara kupitia benki hiyo na kuwaomba Wajasiriamali na Wafanyakazi kutoka taasisi za umma na binafsi kujiunga na benki ya ACB ili kufurahia huduma bora zaidi kwa uharaka, unafuu na usalama.