Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema Wizara ya Maji itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Maji, Nishati na Madini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kwa manufaa ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhandisi Sanga amesema ushirikiano huo umekuwa na manufaa makubwa katika kusaidia kutatua changamoto mbalimbali kwa kujifunza na kubadilishana uzoefu wa kitaalam kati ya Tanzania Bara na Visiwani wakati akizungumza na ujumbe wa Baraza la Wawakilisha la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji Zanzibar (The Consumer Representatives Council) jijini Dodoma.
Wajumbe hao kutoka Zanzibar wamekuja kwa ziara ya kikazi na wanatarajia kutembelea mkoa wa Manyara kujifunza utoaji huduma kwenye miradi ya maji vijijini kupitia Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO’s) chini ya Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).