Home Kitaifa TARURA KAGERA YAFUNGUA BARABARA MPYA KM. 826

TARURA KAGERA YAFUNGUA BARABARA MPYA KM. 826

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Kagera imefanikiwa kufungua  mtandao wa barabara mpya wa Km. 826  katika kipindi cha miaka mitatu kutokana na ongezeko la bajeti.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA mkoa wa Kagera Mhandisi Avithi Theodory  wakati akizungumzia mafanikio ya miaka mitatu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhandisi Theodory alisema kwamba TARURA imefanikiwa kufungua barabara hizo mpya ambazo awali zilikuwa ni changamoto kwa wananchi wa mkoa huo kwani walikuwa wakitembea umbali mrefu kufika eneo la huduma za jamii.

“Tumeweza kuwafungulia njia ambapo awali ilikuwa ni vikwazo kwa wananchi kwani  walikuwa wakitembea umbali mrefu hadi kufikia huduma za kijamii, mfano mtu alikuwa akitembea Km. 21 lakini kwa sasa ni Km. 9, wapo wengine walitembea Km.8 na sasa wanatembea Km. 1.6 , hivyo tumejenga barabara mpya na sasa wananchi hawapati tena shida ya kutumia muda mrefu kufikia huduma za kijamii katika mkoa wetu”.

Aidha, alisema  Mkoa wa Kagera umetengewa bajeti ya fedha shilingi Bilioni 31 mwaka wa fedha 2023/2024 kutoka Bilioni 9  kulinganisha na miaka ya nyuma, jambo ambalo limefanya barabara  za mkoa wa Kagera za vijijini kufunguliwa kwa kasi na kurahisisha maendeleo ya wakazi wa mkoa wa Kagera .

Tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan  aingie madarakani bajeti  yetu imeweza kupanda mara tatu hadi kufikia Bilioni 31 tofauti na bajeti ya  awali  na hivyo kufanya Barabara  za mkoa wa Kagera hususani za  vijijini kufunguliwa kwa Kasi na kurahisisha maendeleo ya wakazi wa mkoa huu” Aliongeza kusema.

Hata hivyo alisema kuongezeka kwa bajeti hiyo imeweza  kuongeza barabara zenye kiwango cha lami Km. 125 kulinganisha  na Km. 80 za awali, ujenzi wa makalavati 1,600 na kufanya  maeneo mengi ya vijijini  kupitika kwa urahisi na hivyo kuweza  kusafirisha mazao yao kutoka kijiji kimoja hadi kijiji kingine na kujipatia kipato.

Pia Serikali kupitia TARURA  itaendelea kuhakikisha wanakuza miji kwa kuboresha miundombinu ya barabara ili wananchi wakiwemo wajasiriamali na wafanyabiashara waweze kusafirisha na kuuza bidhaa zao nyakati zote katika masoko na katika kutekeleza hilo wamefanikiwa kufunga taa za barabarani  zipatazo 240 na nyingine 140 zinaendelea kuwekwa sehemu mbalimbali katikati ya mji.

Naye, Bi. Kudra Kagungu, mkazi wa  Biharamulo  alisema kuwa Serikali inapaswa kupongezwa kwa zawadi kubwa ya kuhakikisha miradi ya barabara inatekelezwa na wananchi wanaondokana na kero katika matumizi ya Barabara mbaya hasa za vijijini.

Alisema uboreshaji wa barabara umeweza kuwasaidia wananchi kujikomboa na umaskini na kuimarika kwa uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja kwani hivi sasa maeneo mengi hakuna tena adha ya usafiri na usafirishaji wa mazao kwani sehemu nyingi ambazo walitumia kiasi cha shilingi elfu 20,000 kufuata mzigo kwa Sasa wanatumia shilingi elfu 3,000 hadi 5,000 kwa sababu barabara zimeimarika.

-Mwisho-

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!