Serikali imeanza kufanya marekebisho ya kubadili muundo wa Baraza la Taifa na Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA).
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Maryam Azan Mwinyi aliyetaka kujua ni lini Serikali itawasilisha Marekebisho ya Sheria ya Mazingira ili kuipa NEMC uwezo wa hadhi ya Mamlaka.
Amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajia kuwa hadi kufikia Juni 2024, Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 uwasilishwe katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua zaidi.
Akiendelea kujibu swali hilo Naibu Waziri Khamis amesema kuwa marekebisho hayo ya kubadili muundo huo ni moja ya masuala yanayopendekezwa kufanyiwa marekebisho ili NEMC iwe Mamlaka.
Akiendelea kujibu maswali ya nyongeza ya mbunge huyo, Mhe. Khamis amesema kuwa miongoni mwa majukumu ya mameneja wa kanda wa NEMC ni kusimamia sheria pamoja na kutoa elimu kwa jamii.
Ametumia nafasi hiyo kuwapongeza kwa utendaji kazi mzuri na kusema kuwa majukumu hayo yanaweza kufanyiwa marekebisho kulingana na sheria itakavypendekeza.
Hivyo, Naibu Waziri Khamis amesema kuwa NEMC itakayofahamika kama NEMA itaendelea kushirikiana kwa ukaribu na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (ZEMA) katika utekelekezaji wa majukumu ili usimamizi wa mazingira nchini uwe endelevu na wenye mafanikio.