Na Shomari Binda-Musoma
IKIWA leo ni siku ya misitu duniani yenye kauli mbiu “Misitu na Ubunifu” Wakala wa Misitu TFS wilaya ya Musoma na ofisi ya mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Sospeter Muhongo wameanzisha kampeni ya kudumu ya upandaji wa miti.
Siku hii ya Umoja wa Mataifa (UN) lengo lake kuu ni kukumbushana umuhimu wa misitu ya aina zote katika uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
UN ilipitisha azimio la siku hii tarehe 21 machi ya kila mwaka kwenye mkutano wake wa tarehe 28.11.2013
Kwa muda wa zaidi ya wiki mbili mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo akishirikiana na mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt Khalfan Haule na Meneja wa Misitu (TFS) Wilaya ya Musoma Boniphace Kaberege wamekuwa wakigawa na kupanda mamia ya miche ya miti ya matunda, mbao na kivuli kwenye shule kadhaa za misingi na sekondari za jimbo la Musoma vijijini huku kampeni hiyo ikiwa ya kudumu
Katika kuhakikisha kampeni hiyo inapata mafanikio TFS Wilaya chini ya uongozi wa Boniphace Kaberege ilitoa mafunzo ya umuhimu wa misitu kwa maisha na ustawi wa jamii mafunzo hayo yalifanywa kwenye shule ya sekondari Suguti ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za mwaka huu.
Wanafunzi na walimu wote wa sekondari hiyo wakiongozwa na mkuu wao wa shule Pendo Kaponoke walihudhuria mafunzo hayo.
Wanavijiji wa Kata ya Suguti (Vijiji 4 vya Chirorwe, Kusenyi, Suguti na Wanyere walihudhuria wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa Kata hiyo Alphonce Wambura
Wanufunzi 100 wa sekondari hii wamekuwa mabalozi wa mazingira chini ya mwalimu wao wa Mazingira Keneth Elias ambao wataongoza kampeni ya upandaji na utunzaji miti ndani ya Kata na Suguti na jimbo zima la Musoma vijijini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake baada ya uzinduzi huo meneja wa TFS wilaya ya Musoma Hamis Boniphace Kaberege amesema kila mwaka wamekuwa wakiotesha miche 350,000 na kuigawa bure kwa wananchi.
Amesema zipo faida mbalimbali za miti ikiwa ni pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,kutunza vyanzo vya maji na kupata mvua za uhakika
Meneja huyo amesema faida nyingine za miti ni kuinua uoto uliopotea na inasaidia kupata maji na hewa safi kwa binadamu na wanyama.
Kwenye mazungumzo yake meneja huyo amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwa namba moja katika suala zima la kuhimiza utunzaji wa mazingira.
Amesema kila wakati Rais Samia amekuwa akihimiza suala la utunzaji wa mazingira kwa maendeleo endelevu na wao kama wasaidizi wake wamekuwa wakiendeleza jitihada zake.
Aidha meneja huyo wa TFS wilaya ya Musoma amemshukuru mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Sospeter Muhongo kwa kuwa mstari wa mbele kuungana na Rais Dkt.Samia kuhifadhi mazingira.
Kaberege ametoa wito kwa wananchi kuwa na utamaduni wa kupanda miti na kuitunza kwenye maeneo yao ikiwemo ya mbao,kimvuli na matunda kwa kuwa ina faida kubwa.