Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya ya Songea Vijijini yaahidi kushughulikia na kuupatia ufumbuzi mgogoro wa ardhi katika kitongoji cha Msiri na Hifadhi ya Maliasili kilichopo katika kijiji cha Nakahengwa.
Kauli hiyo ameitoa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Peramiho, leo tarehe 15/03/2024 katika kijiji cha Nakahengwa Wakati akimnadi Mgombea Udiwani Ndg. Optatus Ndau, ambapo uchaguzi mdogo unatarajiwa kufanyika tarehe 20/03/2024 baada ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo ya Mbinga Mhaule kufariki.
Aliongeza kusema tumejipanga kuhakikisha migogoro yote ya ardhi katika Kijiji cha Nakahengwa inamalizika na watu wanaishi kwa Amani.
“Tunahitaji kuona kila mgeni anayeingia katika Kijiji cha Nakahengwa, hafikirii kuondoka kwa sababu wenyeji wa hapa ni wakarimu na Wenye upendo,” alisema
Katika hatua nyingine Waziri Mhagama amewakumbusha wananchi umuhimu wa kuchagua Mgombea wa udiwani atakayeendelea kuchochea miradi ya maendeleo na kusimamia vyema ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Alikumbusha kuhusu uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2020, tuliomba mchague Mafiga Matatu ya Chama Cha Mapinduzi ili tujipange sawa sawa katika kushughulikia matatizo ya wananchi.
“Serikali kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi imeshaanza kushughulikia bei ya mbolea kwa kuhakikisha inaendelea kushuka ili kusaidia wananchi, ” alibainisha
Muunganiko wa Mafiga haya matatu unaongozwa na Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umesaidia katika kupandisha bei ya mahindi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Songea Vijijini Ndg. Thomas Masolwa amesema ujenzi wa Miundo Mbinu bora ya barabara, Miundo Mbinu ya Afya, Miundo Mbinu ya elimu na Nishati ya umeme inasimamiwa na ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Sasa tunatembea na ajenda ya kuziba pengo katika Kata ya Mbinga Mhalule kwa kutafuta Mtu atakayendelea kusimamia na kuchochea miradi ya Maendeleo kwa Wananchi.
“Kumpigia Kura Mgombea wa Chama cha Mapinduzi ni kupigia Kura maendeleo yanayoendelea kutekelezwa na Serikali,” alibainisha
Naye Mgombe wa Chama Cha Mapinduzi Ndg. Optatus Ndau ameahidi kuendelea kusimamia miradi yote inayotekelezwa katika kata ya Mbinga Mhalule.
Sambamba na hilo Ndg. Ndau ameahidi kuendelea kusimamia migogoro yote ya ardhi ya mashamba na mipaka katika kata ya Mbinga Mhalule.