Na Shomari Binda- Musoma
WAKALA wa barabara (TANROADS) mkoa wa Mara imeliomba jeshi la polisi kuwasaka na kuwakamata wezi wa miundombinu na taa za barabarani.
Kauli hiyo imetolewa na meneja wa TANROADS mkoa wa Mara mhandisi Vedastus Maribe kwenye vikao vya bodi ya barabara na kikao cha ushauri cha mkoa( RCC)
Amesema licha ya TANROADS mkoa wa Mara kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote zipo changamoto za wizi wa miundombinu zikiwemo taa za barabarani.
Katika taarifa yake mhandisi Maribe amesema wapo watu ambao sio waaminifu ambao wamekuwa waking’oa vyuma na kingo za barabarani pamoja na taa jambo ambalo sio jema.
Amesema jeshi la polisi katika kutekeleza majukumu yake waharibifu hao wanapaswa kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Meneja huyo amesema taa za barabarani zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wakiwemo wajasiliamali kifanya shughuli zao wahalibifu hao wamekuwa wakipanda juu ya nguzo na kuiba taa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti licha ya kuendelea kutimiza majukumu yetu lakini kumekuwa na changamoto ya waharibifu wa miundombinu ikiwa ni pamoja na kuiba taa za barabarani”
“Tunaliomba jeshi la polisi kuwasaka watu hawa na kuweza kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine” amesema
Mkuu wa mkoa wa Mara Said Mtanda amesema sio busara kung’oa taa za barabarani kwa kuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi kwenye shughuli mbalimbali ikiwemo ulinzi.
Amesema wananchi pia wanapaswa kuwa walinzi wa kwanza kwa kuwa miundombinu hiyo pamoja na taa zipo kwenye maeneo yao.