Home Kitaifa CHAMA CHA ACT WAZALENDO CHATOA TAARIFA YA MKUTANO MKUU NA VIONGOZI WALIPATA...

CHAMA CHA ACT WAZALENDO CHATOA TAARIFA YA MKUTANO MKUU NA VIONGOZI WALIPATA NYADHIFA

Na Magrethy Katengu

KAMATI Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo imeielekeza Sekretarieti kuandaa midahalo ya wazi ya wagombea wa Chama ikiwemo Ngome za Wanawake na Vijana ili kuwapa nafasi wanachama na umma kwa ujumla ya kuwajua vizuri zaidi wagombea kupitia sera zao.

Hayo yamebainishwa leo Januari 28, 2024 na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa Chama hicho Janeth Rithe akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maazimio ya Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo iliyokutana jana kwenye kikao chake cha kawaida kilichofanyika katika Ukumbi wa Juma Duni Haji uliopo katika Ofisi za Makao Makuu ya Chama, Magomeni, Dar es salaam.

Rithe amesema uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea utakuwa kati ya Februari 14 hadi 24 mwaka huu.

Akizungumzia kuhusu maazimio hayo ameyaainisha kuwa ni pamoja na, chaguzi za mikoa na majimbo, maboresho ya Kalenda ya Mkutano Mkuu Taifa, maboresho ya Katiba ya Chama na Sera ya Usawa wa Kijinsia na 3. Uteuzi wa Makatibu wa Mikoa na Majimbo.

Kuhusu chaguzi za Mikoa na Majimbo, Rithe ameeleza kuwa Kamati Kuu ilipokea Taarifa ya Uchaguzi wa Chama katika ngazi ya Mikoa na Majimbo.

Kwamna kwa upande wa Bara, Majimbo yote 214 yamefanya uchaguzi sawa na asilimia 100 na Mikoa yote ya Kichama 28 imefanya uchaguzi sawa na asilimia 100.

Vilevile, kwa upande wa Zanzibar, Majimbo yote 50 yamefanya uchaguzi sawa na asilimia 100 na Mikoa yote ya Kichama 11 imefanya uchaguzi sawa na asilimia 100. Kamati Kuu imeipongeza Sekretarieti ya Chama kwa kukamilisha chaguzi za Majimbo na Mikoa kwa asilimia 100,”.

Rithe ameeleza kwamba hatua hii ni kiashiria cha wazi cha ukuaji wa kasi wa Chama cha ACT Wazalendo katika kipindi hiki muhimu kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

Kwa upande wa maboresho ya Kalenda ya Mkutano Mkuu Taifa, amesema Kamati Kuu ya Chama Taifa, baada ya kupokea na kujadili Taarifa ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu Taifa, iliidhinisha kuwa Mikutano Mikuu ya Chama ifanyike kama ifuatavyo, Mkutano Mkuu wa Ngome ya Vijana Februari 29, 2024, Mkutano Mkuu wa Ngome ya Wazee Machi1, 2024

Mikutano mingine ni Mkutano Mkuu wa Ngome ya Wanawake Machi 2, 2024, Mkutano Mkuu Taifa Machi 5-6, 2024 huku Mkutano wa hadhara wa Kutangaza viongozi wa Chama waliochaguliwa ukipangwa kufanyika Machi 6 mwaka huu.

Kuhusu, maboresho ya Katiba ya Chama na Sera ya Usawa wa Kijinsia amebainisha kwamba Kamati Kuu imepokea Rasimu ya kwanza ya maboresho ya Katiba ya ACT Wazalendo iliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Chama baada ya kukusanya na kuchambua maoni ya wanachama.

Kwamba Kamati Kuu, baada ya majadiliano ya kina imeelekeza Rasimu hiyo, baada ya maboresho kwa kuzingatia maoni ya Kamati Kuu, ipelekwe Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupokea maoni zaidi kabla haijawasilishwa Mkutano Mkuu Taifa kwa ajili ya kuidhinishwa.

Vilevile, ameeleza kuwa Kamati Kuu imepokea Rasimu ya Sera ya Jinsia inayolenga kuhakikisha uwakilishi mpana zaidi wa wanawake kwenye vyombo vya maamuzi ndani ya Chama na katika chaguzi za kiserikali unazingatiwa. Kamati Kuu imeelekeza kuwa Rasimu hiyo, baada ya maboresho kwa kuzingatia maoni ya Kamati Kuu, ipelekwe Halmashauri Kuu ya Chama Taifa kwa ajili ya kuidhinishwa.

Katika hatua nyingine, Kamati Kuu ilipokea Rasimu ya Sera ya Kuwaenzi Viongozi Wastaafu waliokitumikia Chama kwa heshima, bidii na utii. Baada ya majadiliano ya kina, Kamati Kuu iliridhia Sera hiyo iwasilishwe Halmashauri Kuu kwa ajili ya kuidhinishwa.

Kwenye uteuzi wa Makatibu wa Mikoa na Majimbo, Rithe amesema, Kamati Kuu Taifa kwa kuzingatia madaraka yake chini ya Ibara ya 79 (vii) ya Katiba ya ACT Wazalendo imefanya uteuzi wa Makatibu wa Mikoa ambapo kwa Tanzania Bara ni, Tanga: Mussa Kassim Mbega, Kigoma: Yunus Ruhomvya, Arusha: Bakari Ramadhani na Geita: Reuben John Bujiku.

Wengine ni Kagera: Ladislaus Mujwauzi Kashonde, Njombe: Stanley Mbembati, Morogoro: Vinnie Mtingwa, Dodoma: Sunday Julius Madinda, Mara: Karume J. Mgunda, Mbeya: Athman Mrisho Kabogo, Songwe: Michael Nyilawila, Mwanza: Butije Hamis Butije, Kilimanjaro: Lilian Joseph Mushi, Selous: Mtutura Abdallah Mtutura, Tabora: Hamis Mwandu Mahanga na Ruvuma: Tasilo Milinga.

Kadhalika wengine ni, Iringa: Paulo Simbachawene, Singida: Emmanuel Pius Ipini, Simiyu: Makalanga Tebe, Mtwara: Sharifu Hassan Bilal, Shinyanga: Omary Gindu Gindu, Rukwa: January Yamsebo, Lindi: Faustine Abdallah Khalfan, Manyara: Mwadawa Hamis, Katavi: Bwandu Ndanje, Kahama: Frank Charles Makalanga na Dar es Salaam: Felix Kamugisha. Kwamba Uteuzi wa Katibu wa Mkoa wa Pwani utafanyika wakati mwingine.

Kwa upande wa Zanzibar ni, Micheweni: Khatib Hamad Shehe, Wete: Masoud Juma Mohamed, Chakechake: Saleh Nassor Juma, Mkoani: Khamis Tahir Awesu Moh’d, Kaskazini ‘A’: Sheha Khamis Ali, Kaskazini ‘B’ : Abeid Haji Abdallah, Magharibi ‘A’: Othman Moh’d Abdalla (Mahaja), Magharibi ‘B’: Salim Ali Khamis, Mjini: Mahmoud Ali Mahinda, Kati: Omar Khamis Haji na Kusini: Moh’d Kombo Ali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!