Home Kitaifa GST, TFRA NA TFC YASAINI HATI YA MAKUBALIANO MKAKATI WA KUZALISHA MALIGHAFI...

GST, TFRA NA TFC YASAINI HATI YA MAKUBALIANO MKAKATI WA KUZALISHA MALIGHAFI YA MBOLEA

Mbolea kuzalishwa nchini kwa kutumia Malighafi za ndani

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imesaini hati ya makubaliano (MoU) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Nchini (TFRA) pamoja na Kampuni ya Mbolea (TFC) ya Mkakati wa kuzalisha mbolea kwa kutumia malighafi zinazopatikana nchini.

Hafla ya utiaji saini imefanyika leo januari 25, 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Kilimo uliopo Jijini Dodoma.

Akichangia wakati wa majadiliano, Kaimu Mtendaji Mkuu GST Dkt. Ronald Massawe amesema GST itatoa ushirikiano wa kuhakikisha kuwa taarifa za kina za maeneo yaliyopo malighafi ya madini mbolea zinapatikana na kushauri malighafi ambazo hazihitaji teknolojia kubwa kuziendeleza na kusisitiza kuwa ni vyema mkakati wa uendelezaji ufanyike hadi kufikia hatua ya uzalishaji.

Akitoa wasilisho mbele ya wajumbe wa kikao hicho mjumbe wa Sekretariate inayo ratibu Mkakati huo na kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa GST, Bw. Maswi Solomon amesema, GST imeingia kwenye makubaliano hayo kwa lengo la kutafiti na kubainisha maeneo yapatikanayo madini mbolea ili kuja na mkakati wa uzalishaji wa mbolea kwa kutumia malighafi zipatikanazo nchini.

Aidha, Bw. Maswi amesema, GST haiishii kwenye utafiti pekee ila pia kuainisha sehemu zinazopatika madini mbolea na kushauri nini kifanyike baada ya kugundua maeneo yapatikanayo malighafi hiyo.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TFC Bw. Samwel Mshote amesema, lengo la kusaini makubaliano hayo ni kuangalia ni kwa namna gani taasisi hizo zitashirikiana ili kupata malighafi kwa ajili ya kuzalisha mbolea kwa soko la ndani na nje ya nchi.

Sambamba na hayo, Mshote amesema, mahitaji ya mbolea ni makubwa ambapo zinahitajika tani milioni moja ambapo 10% inazalishwa ndani ya nchi na 90% inazalishwa nje ya nchi.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Bw. Joel Laurent amesema, Tanzania ikiweza kuzalisha Mbolea ndani ya nchi, mahitaji ya fedha za kigeni yatakuwa yanapungua kwa kiasi kikubwa kuliko ilivyo sasa.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli alizipongeza taasisi zilizoshiriki katika hafla hiyo na kuwataka kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo maazimio yote ya kikao hicho.

Pamoja na mambo mengine, hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Madini, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Nishati, GST, TPDC, NDC, STAMICO, Tume ya Madini na TANESCO, Wizara ya Viwanda na Biashara.

#vision2030MadininiMaishanaUtajiri#

#UtafitiwaMadiniTanzania#

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!