Home Kitaifa AMUUA MKE WAKE SHAMBANI WILAYANI BUNDA KWA WIVU WA MAPENZI

AMUUA MKE WAKE SHAMBANI WILAYANI BUNDA KWA WIVU WA MAPENZI

Na Shomari Binda-Musoma

JESHI la polisi mkoani Mara linamshikilia Muyengi Ruben mwenye umri wa miaka 35 mkazi wa Kijiji cha Namhula wilayani Bunda kwa kumuua mke wake Rosemary Maremi kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali juu ya titi la kushoto.

Licha ya kumchoma eneo hilo alimchoma pia nyuma ya bega la kulia na kupelekea kuvuja damu nyingi zilizopelekea kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyptolewa na jeshi la polisi mkoani Mara imesema tukio hilo lilitokea januari 20 majira ya saa 2 asubuhi.

Taarifa hiyo inasema kuwa siku ya tukio mtuhumiwa huyo alimfata mke wake shambani akiwa anapanda mpunga akiwa na watoto wake na kufanya tukio hilo.

Inadaiwa mtuhumiwa alitaka kurudiana na mke wake waliyekuwa wametengana na kukataliwa na kuamua kuchukua uamuzi huo.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mara Salim Morcase ametoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kuzingatia sheria za nchi.

Amesema kunapo kuwa na ugomvi wa kifamilia ni vyema kutafuta ushauri kuliko kujichukulia maamuzi ambayo yanapelekea kuishia mikononi mwa sheria.

Kamanda Moecase amesema maamuzi kama hayo yanapelekea kuwaacha watoto wakiwa hawana malezi ya wazazi na kukosa upendo.

Amesema jeshi la polisi mkoa wa Mara linasisitiza kila mmoja kuzingatia sheria za nchi na kuacha kuchukua maamuzi yasiyofaa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!