Na Magrethy Katengu
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia bajeti yake ya mwaka 2022/2023 itaendelea kuboresha miundombinu ikiwemo bandari,viwanja vya ndege, barabara na madaraja, vivuko na reli kiwa ni pamoja na miradi ya kimkakati ikiwemo mradi wa reli ya kisasa ya SGR.
Akizungumza na Waandishi wa habari Dar es Salaam Waziri wa Wizara hiyo Profesa Makame Mbarawa amsema katika mwaka wa fedha 2022/2023 wizara hiyo imetengewa bajeti ya shilingi trion 1.421 katika sekta ya Ujenzi ,huku katika sekta ya uchukuzi imetengewa bajeti ya shilingi trion 2.135 ambapo fedha hizo zitatumika kukamilisha miradi mbalimbali inayosimamiwa na Wizara yake.
Prof Mbarawa amesema bajeti iliyopitishwa itawezesha sekta ya ujenzi kusimamia miradi ya ujenzi ya barabara,madaraja,viwanja vya ndege,majengo na nyumba za serikali,vivuko pomoja na huduma za ufundi,kuanza miradi mipya pamoja na kukamilisha miradi ya serikali inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
“Tutahakikisha miradi ya Kimkakati ikiwemo ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi (km 3.2) na barabara unganishi zenye urefu wa km 1.66 na ujenzi wa Daraja jipya la Wami (m 513.5);Ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano kwenye majiji upanuzi wa barabara ya Kimara – Kibaha (km 19.2) kutoka njia mbili (2) kuwa njia nane (8), barabara za juu (Flyovers) katika makutano ya Chang’ombe na Uhasibu jijini Dar es Salaam”Amesema Prof Mbarawa
“barabara za mzunguko wa ndani na nje ya jiji la Dodoma (Dodoma Outer Ring Road – km 112.3 & Inner Ring Roads – km 6.3),ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara za kuelekea katika vituo vya reli ya kisasa (SGR) zenye urefu wa kilometa 87.6 katika Mikoa ya Pwani na Morogoro,Ujenzi wa barabara za kuunganisha Bandari ikiwemo barabara ya Kagwira – Ikola – Karema Port (km 112),Kukamilisha kuunganisha mikoa ambayo haijaunganishwa kwa barabara za lami katika mikoa ya Kigoma na Rukwa” alisema Prof Mbarawa
Waziri aliendelea kufafanua kuhusu sekta ya uchukuzi alisema kuwa serikali imepanga kuendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Mtwara, Songwe, Geita, Iringa, Msalato, Musoma na Songea ambapo inatarajiwa pia kuanza utekelezaji wa miradi mipya ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Ndege vya Kigoma, Tabora, Sumbawanga na Shinyanga.
Aidha amendelea kufafanua kuwa serikali inaendelea na maandalizi ya miradi ya ujenzi, ukarabati na upanuzi wa viwanja vya Ndege vya Njombe, Lindi, Mpanda, Lake Manyara, Bukoba, Moshi, Tanga, Simiyu, Mwanza (Jengo jipya la abiria), Arusha pamoja na viwanja vingine vya Ndege vya mikoa.
Pia alibainisha kuwa serikali kupitia wizara hiyo inaendelea kuimarisha usafiri wa Anga ambapo Viwanja vya Ndege vyenye lengo la kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji vinaendelea kujengwa na kukarabatiwa katika Mikoa mbalimbali nchini. Hadi sasa, Serikali ina jumla ya Viwanja vya Ndege 58 vilivyo chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na kimoja kipo chini ya KADCO.
Hata hivyo Prof.Mbarawa amesema kwamba serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeendelea kusimamia Bandari za Mwambao ,pamoja na zile za Maziwa Makuu,ambapo uboreshaji huo katika Bandari ya Dar Es Salaam umefikia katika hatua mbalimbali na kwa sasa kazi ya kuongeza kina na upana wa lango la Kuingilia Meli na eneo la kugeuzia Meli hadi kufikia kina cha mita 15.5 imefikia asilimia 48 lengo ni kusaidia kuondoa foleni za kupakua mizigo.
“kazi ya kuongeza kina hadi kufikia Mita 14.5 na kuimarisha Gati namba 8 hadi 11 taratibu zake zinaendelea vizuri ambapo kazi za upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaji wa nyaraka za zabuni zinaendela ambapo Mtaalam Mwelekezi (Consultant) anatarajiwa kuwasilisha taarifa ya mwisho ya upembuzi mwanzoni mwa mwezi Agosti, 2022 “amesema Waziri
Sambamba na hayo amesema katika mwaka wa fedha 2022/23, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imetengewa jumla Shilingi bilioni 100.112 fedha za nje kutoka Benki ya Dunia (WB) na shilingi bilioni 650.00 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani ya Mamlaka kwa ajili ya kutekeleza kazi mbalimbali zikiwemo Kuendelea kuongeza kina na kupanua lango la kuingilia meli na eneo la kugeuzia meli (entrance channel and turning basin); kuboresha wa Gati Na. 8 – 11 na Gati Na. 12-15 katika Bandari ya Dar es Salaam
Kazi zingine ni kufunga na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na mifumo ya TEHAMA, Kuendelea na kazi za uboreshaji wa Bandari ya Tanga awamu ya pili inayohusisha ujenzi wa gati namba 1 na 2 zenye jumla ya urefu wa mita 450,kukamilisha mradi wa kupanua na kuchimba lango la kuingilia na kugeuzia meli katika Bandari ya Tanga Kuendelea na ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala, Ruvu mkoani Pwani.
Kuhusu ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo Mkoani Pwani Profesa Mbarawa amesema kuwa mwekezaji aliyekuwa anahitaji kuchukua zabuni ya kujenga bandari hiyo ameshundwa kufikia makubaliano na serikali,hivyo serikali inaendelea na mchakato wa kutafuta mwekezaji mwingine ili ajenge bandari hiyo haraka iwezekanavyo.