MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi mkoani Mwanza Marco Lushinge maarufu kwa jina la Smart amesema anatamani kuona jumuiya za chama hicho mkoani humo zinajitegemea kwa kuwa na nguvu za kiuchumi.
Ameyasema hayo jijini hapo katika tukio lililoambatana na kukabidhi Jumuiya ya Wazazi Mkoani Mwanza matofali 1000 na bandari tatu za mabati ili waweze kutumia katika ujenzi wa vitega uchumi vyao katika eneo la Kirumba.
Smart alisema kuwa Jumuiya ya Wazazi ina umuhimu mkubwa katika malezi ya taifa kwani wanayo misingi imara ya uzalendo na mawaidha bora ya kurithisha vijana nchini.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoani Mwanza Mohammed Lukonge alisema wameshaanza ujenzi wa flemu za maduka sita na baadaye watajenga flemu tisa ikiwa ni hatua ya kuifanya Jumuiya hiyo kujitegemea kiuchumi.
Alisema viongozi katika wadhifa wowote wanapashwa kuacha alama hivyo wao wamedhubutu kuanzisha mradi huo baada ya kuona Jumuiya hiyo ikiwa haina mradi wowote kwa mda mrefu ili waweze kuwa na nguvu za kiuchumi zitakazowawezesha kujitegemea.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Fedha wa Jumuiya hiyo Mkoani Mwanza Rahim Jivraj alisema kuwa huo ni mwanzo mzuri katika kusonga mbele kiuchumi ili waweze kujitegemea wenyewe.
Alisema mafanikio hayo yataleta chachu kubwa kwa uchumi wa Jumuiya hiyo na hivyo kuwataka kuongeza juhudi ili wapate mafanikio makubwa ya kiuchumi wafanikiwe katika kazi yao ya kila siku ya kutumikia watanzania.
Mjumbe Baraza la Kuu la Wazazi Taifa AminMohammed Nazmudin Velji alisema anashukuru kuona mitazamo ya chama kuwa na maendeleo endelevu yakifuatwa kwa vitendo.
Aliwataka Wazazi wote kuunga mkono jitihada hizo zilizoanzishwa kwani maendeleo yoyote huletwa na watu wanaojitolea wenyewe badala ya kusubiri kusaidiwa.