NA SCOLASTICA MSEWA, KIBAHA
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema viongozi wa chama hicho wanatakiwa kufanana na Chama chao kimaadili na kiutendaji sambamba na kuheshimu watu.
Kadhalika Nchimbi amesema viongozi wanaotaka kuchaguliwa na Chama hicho wanatakiwa kujitengeneza kufanana na wanaokubalika kwa watu.
Amesema hayo Mjini Kibaha alipokuwa anazungumza na Wanachama wa CCM waliofika kumpokea katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere ambapo amefika kuungana na Makatibu wengine wa kutoka vyama vya Ukombozi Kusini mwa Afrika ambavyo ni ANC cha Afrika kusini, SWAPO cha nchini Namibia, FRELIMO cha Msumbiji, MPLA cha Angola, ZANU – PF cha Zimbabwe na CPC Chama Cha kikomunisty cha nchini China.
“Isifike mahala unakutana na wanachama wanavyokutambulisha kama huyu ni kiongozi wa chama wanaanza kusema huyu nikikutana nae siku za hivi karibuni badala ya kutaja cheo chake,” alisema Balozi Nchimbi.
Alisema wanachama wanatakia kuchagua viongozi wenye sifa wanaoweza kukitetea Chama wenye ambao wanaleta heshima ndani ya chama hicho.
Aliwataka wanachama kutoona haya katika kutetea chama chao ikiwa ni pamoja na kusema mambo ambayo Chama kimefanya kwani hakuna chama kinaweza kufanya hivyo.
“Zipo nchi nyingine watu wanahangaika wanakusanya kodi wengine wanachota wanafanya mambo yao na umasikini unatawala tofauti na CCM yetu,” alisema.
Aliwashukuru wanachama wa chama hicho kwa mapokezi waliyomfanyia huku alisema wakati akiwa Balozi alikuwa anakumbuka chama chake pamoja na kuvaa sare.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao akimkaribisha Katibu Mkuu huyo alisema walipata taarifa ya ujio wake wakaamua kumfanyia mapokezi kwani ni mara yake ya kwanza kufika katika mkoa huo akiwa kama Katibu.
Aidha hafla hiyo ya mapokezi ilihudhuriwa na wanaCCM mbalimbali wa mkoa mzima wa Pwani, viongozi wa CCM mkoa na Wilaya za zote za mkoa wa Pwani akiwemo Katibu wa CCM mkoa wa Pwani Bernard Ghati, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani Mwinyishehe Mlao,
Viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Simon, Katibu tawala wa Wilaya ya Kibaha Moses Magogwa na Mkuu wa Shule ya uongozi ya Mwalimu Julias Nyerere Prof. Marcelina Chijoriga.
+++++++++