Na; Mwandishi wetu
Viongozi wa dini wameombwa kuendelea kusimamia imara na kukemea matendo maovu yanayopelekea mmomonyoko wa maadili hususan kwa vijana hasa katika mazingira ya yanayoendeshwa zaidi na ulimwengu wa kidijitali.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama wakati akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan katika Ibada Maalum ya Kuwekwa Wakfu Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mufindi, Mkoani Iringa, tarehe 07/01/2024.
Waziri amehimiza malezi bora kwa watoto na ikiwezekana jamii kurejea utamaduni wa kitanzania wa mtoto kulelewa na kuonywa na jamii nzima inayomzunguka.
“Serikali inatambua kuwa Viongozi wa dini wana mchango mkubwa katika kuwahimiza wananchi maadili mema na maisha ya uadilifu,” Alifafanua
Waziri amenukuu maandiko Matakatifu kutoka Waraka wa Mtume Paul kwa Wagalatia Sura ya 6: 1-3 yanayosihi kuonya na pale inapobainika mmoja katika jamii amekwenda kinyume kwa kutenda kosa lolote.
Amewaaomba viongozi hao kueendelea kutekeleza jukumu hilo ipasavyo ili kulilinda Taifa dhidi ya janga la mmomonyoko wa maadili.
“Tunaamini kwa kupitia Imani yetu na kukua kwa kanisa, ni kukua kwa Imani ya dini, hivyo kutachochea maadili na kusaidia kupambana na vitendo vibaya vya rushwa na kuimarisha utawala bora” Alibainisha
Aliendelea kusema kuwa, Mambo mazuri yatakayofanywa na washirika wa Dayosisi hiyo yataleta ari na chachu kwa watu wengine ambao sio wanashirika Dayosisi.
Waziri amesema kwamba licha ya Nchi ya Tanzania kutoegemea upande wowote katika masuala ya dini (Secular State) sehemu kubwa ya wananchi wanaamini katika Mungu kupitia dini na madhehebu mbalimbali.
Aidha, Alifafanua kuwa Serikali inaendelea kutambua uwepo wa dini nchini na umuhimu wake katika kulinda tunu za amani na utulivu pamoja na mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za dini katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Waziri ametumia nafasi hiyo kupongeza na kushukuru Kanisa la Kilutheri Tanzania hasa kwa wale waliopata Dayosisi mpya na Mhashamu Askofu Mpya, kuwana matarajio makubwa sana kwa Dayosisi hiyo Mpya.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo la Mufindi Muhasham Baba Askofu Dkt. Anthony Kipangula, amesema kanisa linahitaji kushirikiana na Serikali kutoa elimu ya kujitegemea ili kusaidia vijana kupata ujuzi.
Alisema, Elimu ya Ufundi ni muhimu sana kwa vijana hasa wanaomaliza elimu ya msingi bila kwenda sekondari na wanaomaliza elimu ya sekondari bila kwenda juu zaidi.
“Kanisa linajipanga kuendeleza elimu ya ufundi katika chuo chetu cha Mafinga Lutheran vocation centre ikiwezekana kuanza mchepuo ufundi kama tawi la chuo kikuu kisaidizi cha Iringa,” Alisema
Baba Askofu
Akitoa neno la shukrani Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Mhashamu Askofu Dkt. Fredrick Shoo, ameomba Viongozi wanaomsaidia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumsaidia kwa dhati na kuepuka kuunda makundi ya kumkwamisha.
Tunamuombea Mhe. Rais Dkt, Samia Suluhu Hassani na tunamuunga mkono yeye pamoja na wengine wote wenye mamlaka na nafasi katika nchi yetu.
“Tunaomba kila mmoja asimame kikamilifu katika nafasi yake awatumikie watanzania wasasa na vizazi vijavyo,” alifafanua Mhashamu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.